Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe Neema Mgaya (katikati mstari wa mbele) akiwa na baadhi ya wanawake aliowakabidhi vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Shilingi Milioni 90 Halmashauri ya Makambako Mkoani Njombe ili wajikwamue kiuchumi.
Mbunge wa Viti Maalum CCM mkoa wa Njombe, Neema Mgaya (mbele) akiwa na baadhi ya wanawake aliowakabidhi vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Shilingi Milioni 90 Halmashauri ya Makambako Mkoani Njombe ili wajikwamue kiuchumi.
Baadhi ya vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Shilingi Milioni 90 vilivyolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Neema Mgaya vikiwa tayari kukabidhiwa kwa baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Njombe ili wajikwamue kiuchumi.
Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Neema Mgaya ametoa msaada wa vyerehani
370 vyenye thamani zaidi ya Milioni 90 kwa wanawake mkoani humo ili
wajikwamue kiuchumi huku akiunga mkono juhudi za Serikali inayohimiza
uchumi wa viwanda. Akizungumza Mjini Makambako wakati wa hafla ya
kukabidhi vyerehani hivyo kwa baadhi ya wanawake, Mgaya amesema amefikia
uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kuifanya Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati kupitia viwanda.
Akibainisha zaidi ameeleza juhudi za kumkomboa mwanamke wa mkoa wa
Njombe ni jambo linalopiganiwa kwa miaka mingi hivyo vyerehani hivyo
vitawafungulia njia kuweza kujikwamua kiuchumi.
“Nimekuwa
sina papara katika utendaji wangu, mwaka jana nilitoa msaada wa vitabu
vya ziada kwa Shule za Sekondari Halmashauri ya Makambako, ambapo kwa
mwaka huu nimeamua kuunga mkono juhudi za serikali upande wa viwanda kwa
kuwasadia wanawake hawa vyerehani hivi 370,” alisema Mgaya.
Akifafanua
amesema anatambua thamani kubwa walionayo wanawake hivyo kwa
kuwawezesha vyerehani hivyo kutainua familia na jamii zinazowazunguka
kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia huduma za kijamii na mahitaji
mengine.
“Mtu
ninayemthamini huwa nampa kitu ambacho kitadumu na kumsaidia kwa muda
mrefu, mimi nimeamua kutowapa samaki kwani mtamla ataisha, nimewapa
nyavu ambayo mtaitumia kuvua samaki, nendeni mkavitunze vyerehani hivi
kujiletea maendeleo endelevu,” alisema Mgaya.
Akizungumza
baada ya kupokea cherehani yake Diwani wa Viti Maalum Lupembe Neema
Limbanga amesema alilolifanya Mbunge huyo wa Viti Maalum halijawahi
kutokea katika maisha yake na kwamba vyerehani hivyo vimewafungulia njia
kimaisha.
Naye
Diwani wa Viti Maalum CCM Njombe, Stella Francis amesema Mgaya amewapa
zawadi ambayo licha ya kuwainua kiuchumi itakuwa mkombozi hasa katika
ndoa zao, kwani sasa wataweza kuhudumia familia kwa kushirikiana na
wanaume zao.
Kutolewa
kwa vyerehani hivyo 370 ambavyo ni sawa na viwanda vidogo 92 kwa dhana
ya vyerehani vinne sawa na kiwanda kimoja kidogo kunaufanya mkoa wa
Njombe kuitikia vilivyo wito wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kuhamasisha uchumi wa viwanda. Lengo la Mkoa kupitia wanawake ni kuwa na
viwanda vidogo 35 hivyo kwa vyerehani 370 ambavyo Neema amevitoa ni
kwamba lengo la kimkoa kupitia wanawake limeshafikiwa.