Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukarabati kituo cha afya
cha Laela kilichopo mkoani Rukwa ili kikidhi vigezo vya kuwa Hospitali
ya Wilaya ikiwa ni moja ya jitihada za kupunguza adha ya wananchi
kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya zilipo.
Hayo
yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI,
Mhe. Suleimani Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kwela Mhe.
Ignas Malocha aliyehitaji kujua ni lini kituo hicho cha afya kitapewa
hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mhe.
Jafo amesema kuwa ni uamuzi wa muda mrefu wa Serikali kuiweka Hospitali
hiyo kuwa ya Wilaya na ndiyo sababu ya kufanya jitihada za kukiongezea
uwezo kituo hicho kwa kujenga wodi nyingi pamoja na kutoa kibali cha
kuajiri watumishi wapya kwani kwa sasa kituo hicho kina upungufu wa watumishi .
Amefafanua
kuwa hadi sasa kuna baadhi ya majengo ambayo tayari yameshakamilika
ambayo ni jengo la upasuaji wa dharura, wodi ya wagonjwa waliofanyiwa
upasuaji pamoja na wodi ya mama wajawazito.
“Kwa
sasa kituo cha afya cha Laela hakina miundombinu inayokidhi sifa za
kuwa Hospitali ya Wilaya ila kutokana na kupanuka kwa Mji huo na
kuongezeka kwa watu wanaohitaji huduma katika kituo hicho tumeamua
kukiboresha ili kifikie hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya”, amesema
Jafo.
Ameongeza
kuwa kwa sasa huduma za rufaa kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika kituo
hicho zinatolewa kupitia magari ya kawaida ya Halmashauri kutokana na
ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa lakini Wizara ina matarajio ya
kutenga fedha ya kununulia gari hilo katika Bajeti ya mwaka 2017/2018.
Aidha,
Mhe. Jafo amethibitisha kuwa kituo hicho kimetengewa jumla ya shilingi
9,358,100 katika Bajeti ya fedha ya mwaka huu ambayo itagharamia kununua
dawa na vifaa tiba vitakavyorahisisha upatikanaji wa matibabu kwa
wananchi wa eneo hilo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Dkt Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea
kuipitia mikataba ya makampuni binafsi ili kuangalia namna ya
kushirikiana nao katika kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba katika
Hospitali na vituo vya afya nchini.
0 comments:
Post a Comment