Na Lulu
Mussa
Njombe
Wadau wa Mazingira
wametakiwa kufuata Sera, Kanuni na Tararibu katika kuendesha shughuli zao. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba ameyasema hayo leo Mkoani Njombe
alipokuwa katika mwendelezo wa ziara ya kutembelea Mikoa mbalimbali hapa nchini
kwa lengo la kujionea hali ya mazingira na kutoa maelekezo stahiki.
Waziri Makamba ametoza faini
Kampuni ya TANMAT kwa kuikuka Sheria ya Mazingira inayokataza upandaji wa miti
ndani mita sitini kutoka katika chanzo cha maji. "Kampuni hii imevunja
sheria hivyo hamna budi kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe mfano na kwa
wengine" alisisitiza Waziri Makamba.
Kampuni hiyo imeagizwa
kulipa faini hiyo ndani siku saba na endapo watakiuka hatua kali zaidi za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao. Waziri Makamba pia ameiagiza Kampuni hiyo kuondoa miti
hiyo ambayo si rafiki kwa mazingira mapema iwezekanavyo na kuagiza Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwapa 'Restoration
Order" kurudisha mazingira katika
hali yake ya kawaida.
Katika hatua nyingine,
Meneja wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na upandaji wa miti Bw. Joseph Shirima
amekiri kupokea barua zizoelekeza kusitisha uharibifu huo wa Mazingira katika
chanzo cha Mto Mbukwa ambacho kinasambaza maji kwa wakazi wengi wa Wilaya ya
Wanging'ombe.
Aidha, Waziri Makamba
ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Njombe kupitia Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema
Nchimbi kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachi kuacha kulima bustani za
mbogamboga pembezoni mwa mito.
Dkt. Nchimbi alimfahamisha
kuwa kwa sasa kuna kikundi kijulikanacho kwa jina la "Jerusalemu"
kinachotoa mafunzo kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha
uhifadhi wa mazingira ambapo lengo ni kuanzisha vituo kama hivyo vya mafunzo
kwa Halmashauri zote za Mkoa huo.
Waziri Makamba alitembelea
na kuona "vinyungu" ambavyo awali vilikua vikilimwa kando ya mito na kwasasa
vimehamishiwa majumbani, katika kuunga mkono jitihada hizo njema Waziri Makamba
amechangia mifuko Hamsini ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa
litakalotumika kutoa mafunzo zaidi ya kilimo.
Waziri Makamba Waziri
Makamba anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya mazingira nchini,
hii leo amewasili katika Mkoa wa Mbeya.
0 comments:
Post a Comment