SERIKALI inapitia upya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili
kuangalia changamoto zilizomo. Mapitio hayo yatakamilika kabla ya
Desemba, mwaka huu, lengo likiwa kutoa fursa kwa wadau kushirikiana na
serikali katika suala zima la ajira nchini.
Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na
Ajira, Ally Msaki alisema hayo jijini Dar es Salaam hivi karibuni na
kuongeza kuwa hatua ya kuipitia sera hiyo, inatokana na kuwapo kwa
mabadiliko mbalimbali.
Alisema, serikali itafanya kila linalowezekana, kuhakikisha
kunakuwepo sera, sheria pamoja na kanuni rafiki, kwa maendeleo ya
programu zinazokuza ujuzi na ajira kwa vijana.
“Sera hiyo imekuwa ikipitiwa na Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa
Umaskini (Repoa) na tayari ripoti inayoelezea hali halisi,
imeshajadiliwa na wadau na sasa hivi wanaandika sera yenyewe,” alisema
Msaki.
Alisema wadau, wameshiriki katika kuipitia sera hiyo, kazi kubwa
imefanyika na imeangalia changamoto na matatizo mbalimbali yanayoikabili
sera hiyo ili itakapokamilika itatoa mwanga wa wadau wengine
kushirikiana na serikali katika suala la ajira.
Msaki alisema serikali itaendelea kusimamia sera hiyo ya elimu na
mafunzo ya ufundi stadi, kwa lengo la kuweka msisitizo katika kuandaa
mazingira na kutoa elimu ya ufundi stadi katika ngazi mbalimbali
kuendana na mahitaji ya soko la ajira na hatimaye kuongeza ajira nchini.
Kuhusu mipango ya serikali katika juhudi za kukuza ajira, ni pamoja
na kuimarisha utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya vijana ambao unalenga
kuwasaidia vijana kujiajiri na kuwapa mikopo ya masharti nafuu na
mafunzo ya ujasiriamali.
Alisema serikali itajikita katika kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji
kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia
40 ya nguvukazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020,
kulingana na mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia
2016/17 hadi 2020/21.
0 comments:
Post a Comment