Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu.
Aliyasema hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana wakati wa
kikao cha kazi baina yake na Wajumbe wa Baraza la Uwezeshaji la Baraza
la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), akiwamo Katibu Mtendaji
wa Baraza hilo, Beng’i Issa na Mwenyekiti wa Bodi, Omari Issa.
Baadhi ya ajenda kwenye kikao hicho ilikuwa ni kupata na kujadili
taarifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi Tanzania, fedha za mpango wa
uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira na uzinduzi wa mkakati wa
sekta mbalimbali wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Dk. Nagu alitoa wito kwa NEEC kukutana na Chama cha Wenye Benki
nchini na kuwashawishi waone umuhimu wa kutumia sehemu ya faida yao
katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kwenye miradi ya biashara.
“Tangu mfuko wa uwekezaji uanzishwe, haukui na sababu ni kwamba
unategemea chanzo kimoja tu serikali, sasa lazima tuondokane na mawazo
ya kuitegemea serikali tu tuwe na vyanzo vingine vya mapato na
tukikutana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, naamini watakuwa tayari
kuchangia jitihada hizi za serikali,” alisema.
Aidha, alisema vikundi vya kuweka na kukopa maarufu kama vicoba,
vikisimamiwa na kuendeshwa vizuri, vitakuwa mkombozi mkubwa wa uchumi
wa Tanzania na kuwakwamua wananchi wengi kuondokana na tatizo la
umaskini kwa kuanzisha miradi.
Waziri Nagu alisema kuna ushahidi wa baadhi ya wananchi
walioanzisha na kusimamia vizuri vicoba na hivi sasa wana mitaji mikubwa
inayowawezesha kufanya biashara kubwa na kuongeza mitaji.
“Kuna mfano dhahiri wa kikundi cha watu 30 ambao wamefanikiwa
kukusanya Sh. milioni 300 ndani ya muda mfupi, sasa kama watu 30 tu
wanaweza kukusanya kiasi hicho cha fedha, si jambo la kubeza, inaonyesha
kwamba tukivisimamia vizuri vitawakomboa wananchi wengi kiuchumi,”
alisema.
Alisema iwapo wananchi watajiunga na vicoba na kuwekeza kwenye
miradi inayowapa faida ni dhahiri wananchi wengi watakata tamaa ya
kujiunga na vikundi hivyo lakini kama vitakuwa vikijiendesha kwa hasara
hakuna atakayejiunga.
"Kwa bahati nzuri vicoba ni watu wanaofahamiana na wanaoaminiana na
wakipata mwongozo mzuri naamini kabisa watafika mbali zaidi, ndiyo
sababu nimeona umuhimu wa kumjumuisha Mwenyekiti wao Taifa, Devotha
Likokola, kwenye baraza hili, kwa sababu naamini kabisa kupitia Vicoba
tunaweza kufika mbali zaidi kiuchumi,” alisem Dk. Nagu.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.