Kata ya Iwawa ilipo shule hiyo.
Na Edwin Moshi wa Globu ya Jamii, Makete
Wafunzi
wa shule ya sekondari Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe wamekiri
uwepo wa wanafunzi wenzao ambao wanajihusisha na vitendo vya ngono na
wengine wanaishi na virusi vya UKIMWI, licha ya jamii kudhani kuwa
wanafunzi hawawezi kuwa na virusi hivyo kwa minajili kwamba bado ni
wadogo.
Hayo
yamebainika baada ya mtandao huu kufanya mahojiano ya kina na baadhi ya
wanafunzi wanaosoma shuleni hivi karibuni kwa ruhusa ya mkuu wa shule
hiyo Bw. Christopher Haule hapo kufuatia wananchi wengi wilayani hapo
kudhani kuwa wanafunzi hao hawana maambukizi ya vvu kwa kuwa ni wadogo
na huwenda hawajaanza kujihusisha na vitendo vya ngono.
Mwanafunzi
mmoja (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) amesema ana marafiki
zake zaidi ya watano ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI na hajui
walivipataje, hivyo anaamini wapo wanafunzi wengi ambao wana maambukizi.
Amesema
jamii inapaswa kuondokana na dhana potofu kuwa mabinti ama vijana
wadogo hawana vvu waache mara moja kwa kuwa virusi vinampata mtu yeyote
bila kujali umri.
“Mtu
anayedhani kuwa wanafunzi huwa hawana vvu ni uongo, na pia waanatakiwa
kuacha kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kwa madai kuwa hawana vvu,
lakini wakumbuke sheria za nchi haziruhusu kujihusisha kimapenzi na
wanafunzi, jamani Ukimwi upo kwa kila mtu” alisema mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi
mwingine amesema yeye hafahamu kama wanafunzi hao wenye vvu
wanajihusisha kimapenzi na watu kwa kuwa wapo ambao wanaishi na wazazi
wao na wengine wamepanga kwenye nyumba maarufu kama mageto ambao kwa
kiasi kikubwa wako huru kufanya mambo yao kwa kuwa hawana muangalizi.
“Ni
kweli kabisa wapo wanafunzi wenye vvu wanaoishi wenyewe kwenye mageto,
lakini mimi sijui kama wana wapenzi ama lah, maana ni ngumu kujua na
mimi sipo hapa kwa ajili ya kufuatilia maisha ya mtu, na hao ninao
kwambia kwa kuwa ni marafiki zangu na waliwahi kuniambia kuwa wanaishi
na vvu” alisema mwanafunzi huyo(jina tunalo)
Mmoja wa mwanafunzi aliyezungumza na mtandao huu
Mwanafunzi upande wa kushoto wa picha hii amemweleza mwandishi wetu kuwa mpenzi wake anamlazimisha kufanya mapenzi bila kondomu
“Mimi
kwa upande wangu Kusema kweli nina mpenzi na nilishawahi kupima vvu
mwaka jana (2012) na kujikuta sina maambukizi namshukuru Mungu kwa hilo,
na pia nimekuwa nikifanya mapenzi kwa kutumia kondomu lakini kuna
wakati mwingine hatutumii mimi na mpenzi wangu na mara nyingi yeye
ndiyo ananishawishi tusitumie, na huyo mpenzi wangu si mwanafunzi ni
jamaa tu wa pale mtaani kwetu, na mimi huwa nakwenda home kwake(Nyambani
kwake) na wakati mwingine anakuja geto kwangu, ili atumie kondom huwa
namwambia leo ni siku zangu za hatari, hapo ndipo atavaa kondomu”
alisema mwanafunzi huyo wa kike ambaye anaishi kwenye nyumba ya
kupanga.
Akizungumzia
suala hilo, diwani wa kata ya Iwawa Benjamin Mahenge alikiri kuwepo kwa
tatizo la ukimwi kwa kila mtu, na kuongeza kuwa hata wanafunzi wapo
wenye vvu ingawa ni kwa kiasi kidogo ukilinganisha na miaka iliyopita
na pia wapo wanafunzi wanaojihusisha na vitendo vya ngono, na ambao
wameshabainika wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria
Diwani wa kata ya Iwawa Benjamin Mahenge (kushoto) akizungumza na mwandishi wa habari hizi
"Unajua
ni ngumu mwanafunzi kuniambia mimi ama kiongozi mwingine kuwa
anajihusisha kimapenzi na mtu lakini kwako mwandishi kasema, mimi
ninaomba wawe wawazi ili tuweze kuwasaidia hasa pale linapojitokeza
tatizo hasa mimba kwa kuwa hawawataji wahusika" alisema Mahenge
Mahenge
amesema huu ni muda wa jamii kubadilika na kuondokana na dhana potofu
kuwa wanafunzi hawawezi kuwa na vvu, na pia wawaache wanafunzi hao
wasome na si kuwarubuni na kujikuta wakifanya nao mapenzi
Pia
amesema wapo wanafunzi katika kata yake ambao wamepanga na uangalizi
wao si mzuri kwa kuwa wanajiamulia mambo yao wenyewe hata kama si mazuri
kutokana na kukosa uangalizi wa watu wazima.
“Unakuta
mwanafunzi kajipangia kwenye chumba chake, yeye ndio kila kitu, akitaka
kusoma haya, akitaka kwenda disco hakuna wa kumuuliza, hii ni hatari
pia” alisema Mahenge
Moja ya nyumba iliyoko Makete mjini amayo wanafunzi wamepanga
Kwa Hisani ya Edwin Moshi