WANAUME WATAHIRIWA KUEPUKA UKIMWI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SERIKALI wilayani hapa inaendelea kuwafanyia tohara wanaume wasiotahiriwa ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kuzuia kuongezeka kwa maambukizi mapya ya Ukimwi kwa wakazi wake.
Hatua hiyo imetokana na wataalamu kubaini kuwa, kuna uhusiano mkubwa kwa wanaume wasiotahiriwa na ongezeko la maambukizi mapya ya Ukimwi.
Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa wilaya hiyo ina asilimia 6.1 ya maambukizi na Mkoa wa Njombe ndiyo unaoongoza kitaifa kwa kuwa na wastani wa asilimia 7.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Madaha, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusu mkakati wa kupambana na maambukizi mapya ya ugonjwa huo ambapo kwa sasa umepata mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa Madaha, Wilaya ya Ludewa ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa kwa Ukimwi na kunatakiwa juhudi kubwa na za makusudi kupunguza tatizo hilo ikiwamo kuongeza elimu ya uelewa wa athari kwa wananchi.
Alieleza kuwa, hapo mwanzo mapambano dhidi ya Ukimwi yalikuwa magumu na tatizo kubwa lilionekana kuwepo kwa idadi kubwa ya wanaume wasiotahiriwa hivyo kwa namna moja na nyingine kuchangia kuongezeka kwa tatizo.
Madaha alisema, pamoja na hatari ya kupata Ukimwi kwa urahisi, lakini pia kutofanyiwa tohara kwa wanaume kunasababisha maambukizi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake jambo ambalo ni hatari kwa afya na kusababisha vifo.
Aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuwa waangalifu na nyendo zao na kujiepusha na tabia inayoweza kuwasababishia kupata maambukizi mapya kwa kuepuka kufanya ngono zembe.
Chanzo;Habari Leo 

MCHAKATO WA KATIBA MPYA: TULIJIKWAA WAPI NA TUTOKE VIPI-2

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
Kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza, kuna kasoro kwenye mchakato wa Katiba Mpya unaondelea nchini lakini Tume ya jaji Warioba, hususan Rasimu, ina uhalali mkubwa zaidi wa kisheria na hata wa kisiasa.
Kuhitimisha, ni hili la ushirikiano uliotolewa kwa Tume ya Warioba na taasisi za kikatiba na kiserikali. Taarifa rasmi za tume zinathibitisha kuwa kati ya taasisi tajwa zilizotoa maoni yao kwa Tume na kwa maandishi, ni Bunge la Jamhuri, Baraza la Wawakilishi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na mengineyo mengi.
Kifungu cha 18 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kilitoa fursa kwa taasisi tajwa kujigeuza kuwa ‘Mabaraza ya Katiba’ na “kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba”. Ni muhimu hili likatiliwa maanani na maoni haya yakajulikana, tukizingatia dai la mara kwa mara kuwa Tume haikukusanya maoni ya Watanzania ‘ya kutosha’.
Tulijikwaa Wapi?
Wahenga walinena: Angalia ulipojikwaa, siyo ulipoanguka. Ile siku baadhi ya wajumbe, hususan wale waliomo katika kundi linalojulikana zaidi kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliposusia kikao na kutoka nje ya Bunge Maalumu, mchakato ulikuwa umeaungukia pua, hata kama siyo ‘kifo cha mende’.
Lakini, tulijikwaa wapi? Ni nini, na vipi tukajikuta katika mkwamo huu? Tuelewe kuwa Bunge Maalumu ndio chombo kitakachopitisha ile Rasimu ya Katiba ambayo hatimaye itapigiwa kura ya maoni. Hivyo ndivyo inavyosema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika ‘Sehemu ya Sita’.
Kwa hiyo, kisheria, hata kisiasa, Bunge Maalum ni sehemu nyeti na muhimu katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya, Katiba ambayo itarekebisha ule upungufu, uliomo katika ‘Sheria Mama’ iliyopo. Na kwa kufanya hivyo, kuhitimisha mambo mawili: Kuandika Katiba Mpya na kusimika misingi mipya ya utawala (bora) wa Taifa letu.
Kwa mtazamo wangu, na kwa ujumla wake, tulianza vibaya! Na hili linajidhihirisha tukikubali tathmini ifuatayo. Uzoefu unaonyesha kuwa uongozi wa nchi ulikuwa na dhamira thabiti kukabili upungufu sugu ya ‘Sheria Mama’ uliopo. Kwamba, badala ya kuendelea na utaratibu wa ‘kupiga viraka’ Katiba iliyopo ya 1977, ni bora tukachanja mbuga mpya, kwa mantiki ya mchakato mpya, na mpana zaidi, wa kupata mustakabali mpya wa Katiba. Na ndiyo maana kila mtu aliyeisikia ile kauli ya Rais Kikwete siku ile ya Desemba 2010, alijawa na faraja na matumaini makubwa. Sikumbuki kusikia hata sauti moja ya kupinga wala kuhoji kauli lile.
Lakini uzoefu umekuja kutonyesha kuwa ‘dhamira’ ilikuwa kionjo muhimu, lakini siyo pekee, katika kufanikisha zoezi la kupatikana Katiba Mpya na iliyo bora zaidi, kwani hata safari ya kwenda jehanamu, inapitia juu ya njia ya ‘dhamira njema’!
Tulianza vibaya pia, kwa kuchomeka kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kifungu 36 (5). Kinanena: “Endapo wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘Hapana’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, itaendelea kutumika”
Je, huu si uchuro (nuksi)? Inakuwaje tunakiri kuwa ‘Sheria Mama’ iliyopo ina upungufu wa kimsingi, na papo hapo kuweka uwezekano wa kisheria wa ‘kumeza matapishi yetu’? Taifa limeingia gharama kubwa ajabu (inasemekana, ni zaidi ya Sh100 billioni), lakini hatima ya yote, ni kujikuta pale pale tulipokuwa (‘back to square one’), kabla ya mchakato kuanza!
Ukiachilia mbali uchuro huo, ushahidi zaidi wa jinsi tulivyoaanza vibaya, uko pia katika mambo mawili makuu yafuatayo. Mosi, tulikwepa kujipa nafasi ya kuijadili kwa pamoja na kwa kina, ‘Sheria Mama’ iliyopo. Kwa kujinyima fursa hiyo, tulijinyima nafasi ya kuwa na maridhiano kuhusu ni kipi kizuri kwenye Katiba ya mwaka 1977 (na kwa hiyo kinahitaji kulindwa, na kuendelezwa), na ni masuala gani yamegubikwa na utata (na hivyo, yajadiliwe kinagaubaga, mwuafaka upatikane na tusonge mbele). Hili pengine ndio lingetusukuma kujiuliza, na kupata mwafaka wa swali nyeti: Muungano umekuja na faida gani kwetu sote? Tuendelee kuuenzi Muungano kwa mikakati ipi?
‘Kosa siyo kufanya kosa. Kosa ni kurudia kosa’. Na wala kuanguka sio dhambi, ili mradi utafute pale ulipojikwaa. Tukifanya hivyo, tutaweza kujikwamua. ‘Kosa’ letu kubwa kwa mantiki hii, ni ‘kuanza vibaya’. Mosi, tumeingia kwenye mchakato wa kutafuta Katiba Mpya, pasi kuichambua ‘Sheria Mama’ iliyopo, ili kubaini na kukubaliana juu ya nini hasa kiwe ‘moyo’ wa hiyo Katiba mpya tuitakayo. Pili, mchakato umesimikwa kwenye Sheria (Sura ya 83) yenye utata wa kisheria na wa kisiasa. Tatu, badala ya ‘Bunge Maalum la Katiba’ tumeunda ‘Bunge Maalum la Wanasiasa’. Nne, dhamira njema ya kupata Katiba mpya, imetiwa nuksi na Kifungu 35 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Chanzo;Mwananchi

`JAMII FICHUENI MTANDAO WA UFADHILI MAUAJI ALBINO`

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi
 
Maaskofu na mamia ya wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini wanaohudhuria kongamano la maombi katika mji mdogo wa Makambako mkoani Njombe, wameitaka jamii nchini kusaidia kuufichua   mtandao wa wafanyabiashara wanaofadhili wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Kauli ya Maaskofu na wanamaombi hao imekuja siku mbili tangu Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, kuelezea masikitiko yake juu ya vitendo viovu wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Baadhi ya mikoa waliyotoka maaskofu na wanamaombi hao ni ya Mbeya, Iringa, Mwanza, Shinyanga, Tanga, Kilimanjaro, Mara, Arusha, Morogoro, Ruvuma, Dodoma na Rukwa.

Maaskofu na wanawake hao, wamewalaani wauaji na watu wanaoufadhili mtandao huo wakisema   wanajulikana kwani wanaishi hapa nchini.

"Sisi tunaamini kama viongozi wa serikali watasimamia kikamilifu kukabiliana na unyama huu wa mauaji ya albino, itashinda," ilisema sehemu ya tamko lao lililosomwa na Askofu Msaidizi wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste nchini, Mchungaji William Mwamalanga.

Aidha, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete, kutangaza mauaji ya albino janga la kitaifa.
 
CHANZO: NIPASHE

MTOTO WA KITANZANIA ASHINDA INSHA SADC

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATOTO wa Kitanzania kutoka shule za kawaida na zile za kata, wameendelea kuipa nchi heshima kimataifa, kwa kuongoza katika mashindano ya kitaaluma.
Jana mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Naboti iliyopo Makambako mkoani Njombe, Neema Mtwanga (16), aliibuka mshindi wa kwanza miongoni mwa washindani 39 katika Shindano la Utunzi wa Insha, lililoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).
Huo ni ushindi wa pili kwa watoto wa Kitanzania kimataifa, baada ya Peter Kilave, ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Tushikamane ya mjini Morogoro, kushinda tuzo ya Insha bora katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka jana.
Ushindi wa Neema ulitangazwa jana katika mji wa kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe, kunakofanyika mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC. Neema alipongezwa na Rais Jakaya Kikwete, aliyepo nchini humo kuhudhuria mkutano huo.
Kutokana na ushindi huo, Neema alitunukiwa tuzo ya ushindi huo, hundi ya dola za Marekani 1,500 ambayo ni sawa na Sh milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC.
Pia, amepewa zawadi ya Ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama). Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe.
Nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland. Insha 39 zilipokewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC, ikiwa ni insha tatu kwa kila nchi.
Insha hizo zilitoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zamibia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, mwezi Julai mwaka huu kupitia insha zote na kutoa uamuzi wa washindi.
Mkuu wa Shule
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Akulasi Kyando alisema amepokea kwa furaha ushindi huo na hasa baada ya Neema kuzingatia maelekezo waliyompa.
“Tumefurahi, tena ameitangaza shule, tulimpa moyo kwa kuwa tunamfahamu ni mwandishi mzuri mpaka hata nyie mmemfahamu,” alisema.
Mwalimu Kyando alisema Neema ni mwanafunzi mwenye tabia nzuri na kwa kudhihirisha hilo, yeye ndiye Dada Mkuu wa shule hiyo.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu huyo, hata katika taaluma, Neema amekuwa na matokeo mazuri na hata mtihani wa mock wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni, alipata daraja la kwanza.
Mtoto wa mkulima
Gazeti hili lilitaka kujua mazingira anayotokea Neema, ambapo mwalimu wake alisema anatoka kijijini katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa na kuongeza: “Ni kijijini na ni mtoto wa mkulima tu.” Ofisa Elimu wa Mkoa wa Njombe, Said Nyachiro, alisema ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa shindano hilo na kupeleka kwa wakuu wote wa shule zilizopo katika mkoa huo.
Alisema mbali na kusambaza taarifa hizo katika mabango, wamekuwa wakiwasihi walimu kusaidia wanafunzi wenye uwezo, kushiriki katika mashindano hayo. Alisema amefurahi baada ya kupata habari za mwanafunzi kutoka Njombe, kuongoza nchi 13 za SADC.
Masharti ya insha Wanafunzi waliopenda kushiriki katika shindano hilo, walitakiwa “Kutoa mapendekezo ya nini kifanyike katika sekta ya elimu, ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa vijana”.
Katika utangulizi wa insha hiyo, mwanafunzi alitakiwa kuhakikisha anamvutia msomaji kwa kutambulisha mada na kuanza kujadili. Msisitizo katika utangulizi, ulikuwa kumtambulisha msomaji mada na kumuingiza katika mjadala.
Alitakiwa kueleza namna anavyofahamu mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la joto duniani, kwa kutoa utambulisho wa moja kwa moja katika aya moja au mbili tu.
Katika kujadili, mwanafunzi alitakiwa kuanza kujadili mada kwa kufuata utaratibu uliowekwa bayana, na aliruhusiwa kuweka vichwa vya habari kwa ufupi kutoka hoja moja kwenda nyingine.
Usahihishaji
Katika utaratibu huo wa usahihishaji, wanafunzi walitakiwa kujadili kwa kuzingatia mgawanyo wa sehemu tano muhimu za insha hiyo na waliruhusiwa kuweka vichwa vya habari kwa ufupi, kutambulisha sehemu husika.
Sehemu ya kwanza ya insha hiyo, ilipaswa kuelezea sababu za mabadiliko ya tabia nchi, ilikuwa na alama kumi kati ya alama mia moja za insha nzima.
Sehemu ya athari za ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ilipewa alama 20 kati ya alama mia moja za insha hiyo.
Aidha, sehemu ya kwanza kwa alama nyingi ni mafanikio na wapi paliposhindikana katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kyoto, uliotaka nchi zenye viwanda kupunguza utoaji wa hewa ukaa ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2005.
Sehemu hiyo ilikuwa na alama 25. Pia mwanafunzi alitakiwa kueleza changamoto katika kushughulikia athari za mabadiliko ya tabia nchi na sehemu hiyo ilikuwa na alama 20.
Sehemu ya mwisho kabla ya hitimisho, ambayo nayo imepewa alama nyingi yaani 25 kati ya 100, mwanafunzi alitakiwa kutoa ushauri nini kifanywe na sekta ya elimu katika nchi za SADC ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wanafunzi wote waliopenda kushiriki, walitakiwa kuwa makini na alama zilizopangwa katika kila sehemu, hivyo wasahishaji walitarajia aya ziwe nyingi katika sehemu ambazo zimewekewa alama nyingi.
Katika hitimisho la insha hiyo, mwanafunzi alitakiwa kueleza kwa ufupi hoja muhimu alizozitetea katika mjadala na alipaswa kuweka msisitizo kuhusu nini angependa kifanywe na nchi wanachama wa SADC katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi katika Ukanda huo.
Wanafunzi pia waliwekewa onyo kwa msisitizo dhidi ya atakayeiga insha kuwa ni kola la kitaaluma. Lakini pia waliruhusiwa kuomba ushauri kutoka kwa walimu na kufanya marejeo kutoka katika vyanzo vinavyotambulika.
Chanzo;Habari Leo

WAMAHIAJI HARAMU 21 WAKAMATWA NJOMBE WAKIPENYA KWENDA NCHI ZA KUSINI MWA TANZANIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Hawa  ni  raia  wa  Ephiopia ambao  walikamatwa  Makambako  Njombe  jana
hapa  wakipata  chai  baada ya kukamatwa
Hivi  ndivyo  walivyokuwa  wakiishi katika  lori  hilo
Hili  ndilo  lori  lililokuwa  likiwasafirisha na  dereva  wake  kukimbia
Ofisa uhamiaji  Njombe  akiwapa  chai wahamiaji hao
 Chanzo francis Godwin Blog

WAKULIMA WAHAMASISHWA KUUNDA VIKUNDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

KITUO maalumu cha uendelezaji kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kimetoa wito kwa wakulima wadogo kuungana kwa kuunda vikundi vidogo ili kuirahisishia Serikali kuwafikishia huduma muhimu za pembejeo na mikopo katika kuinua sekta hiyo hapa nchini.

Wito huo ulitolewa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo hicho, Geoffrey Kirenga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mada alizotarajia kuziwasilisha kwenye mkutano wa wadau wa Umoja wa Watendaji Wakuu wa Kampuni (CEOrt).

"Mkiungana pamoja inakuwa rahisi kuwapatia mafunzo na kuwawezesha kupata mikopo, kwa sababu jukumu letu ni kuwatafutia masoko na kuwawezesha wakulima hawa kuongeza uzalishaji," alisema kirenga.

Aidha alitoa wito kwa wawekezaji na kampuni binafsi kuwekeza kwenye sekta ya kilimo katika ukanda huo kwa kuwa ni ukanda ambao una hali ya hewa nzuri inayostawisha vyema mazao mbalimbali yanayotakikana.

"Kwa mfano maeneo ya Mkoa wa Iringa wanalima pia viazi, awali walikuwa wakivuna kuanzia tani 5 hadi 7 kwa mwaka lakini baada ya kutafuta wawekezaji na kuwasaidia wakulima wadogo na wa kati, sasa wanavuna tani 25 hadi 30 za viazi.

Alisema ukanda huu unazalisha mazao ya chakula na biashara kwa asilimia 65 nchini, sasa iwapo zikitumiwa ipasavyo fursa zilizopo katika ukanda huu hawawezi kuhangaika hata kidogo.

"Kwa sababu tulijaribu katika shamba la mpunga hapo Kilombero kwa kutafuta mwekezaji ambaye aliwasaidia wakulima, na sasa matunda yanaonekana kwani wanavuna tani 5.6 za mpunga kutoka tani moja za awali walizokuwa wakivuna," alisema Kirenga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CEOrt, Ali Mufuruki alisema jukwaa hilo litaendelea kuwakutanisha wataalamu mbalimbali na maofisa watendaji wakuu wa makampuni ambao ni wanachama ili kuisaidia serikali kujikwamua kiuchumi.

Alisema ndani ya jukwaa hilo la CEOrt kuna kampuni zaidi ya 100 ambazo kwa hakika zikitumiwa vyema zinaweza kuinufaisha jamii inayowazunguka

Chanzo;Majira

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa