Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Gerson LwengeAkizungumza
katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa
na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa
na Televisheni ya Taifa (TBC)
Na. Aron Msigwa -Dar es salaam.
Serikali
imesema kuwa itaendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watendaji
wa sekta ya maji watakabainika kujihusisha na vitendo vinavyohujumu miundombinu
ya maji kutokana na maslahi binafsi na kusababisha wananchi kukosa huduma maji
katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza
katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa
na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa
na Televisheni ya Taifa (TBC) leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema baadhi ya watumishi wasio waaminifu
wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu na miradi mipya ya
maji inayoanzishwa na Serikali ili waweze kunufaika na biashara ya kuuza maji.
Amesema
Wizara yake imekwisha kuwasimamisha kazi Mameneja 9 waliokuwa wakihushishwa na
wizi wa kimtandao wa maji katika maeneo mbalimbali hususani katika jiji la Dar
es salaam.
‘’
Nimewasimamisha Mameneja karibu 9 waliokuwa wakihusika na wizi wa kimtandao wa
maji na kuwafanya wananchi wakose huduma hii kwa muda mrefu, ninaomba wananchi
watoe ushirikiano ili tuwakomeshe wahujumu hawa, tunahitaji kuondoa hali hii
kwa kuwa maji ni uhai wa Taifa’’ Amesisitiza
Amewaomba
wananchi waendelee kutoa taarifa kwa
mamlaka zinazohusika pale watakapobaini vitendo vinavyoihujumu sekta hiyo ili ili
hatua stahiki kwa wahusika zichukuliwe ikiwemo kuwafikisha mahakamani wale wote
wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa maji na kuwafanya wananchi wawe na malalamiko
ya kukosa maji.
Akizungumza
kuhusu vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya maji nchini
amesema kuwa kiasi cha shilingi Trilioni moja kimetengwa kwa ajili ya kuboresha
huduma ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini.
Amesema
lengo la Sera ya Maji ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi
ndani ya umbali wa mita 400 jambo ambalo linaendelea kutekelezwa na kuongeza
kuwa tayari miradi ya maji 1200 kati ya 1800 mijini na vijini imekamilika na
kuwezesha asilimia 72 ya wananchi vijijini kupata maji na asilimia 80 ya
wananchi walio mijini kupata huduma hiyo.
Amesema
Serikali imejitahidi kuwekeza kwenye miundombinu mikubwa ya maji katika maeneo
ya mijini hasa katika mikoa yenye idadi kubwa ya watu ikiwemo jiji la Dar es
salaam, Mbeya, Mwanza na miji mingine na kuongeza kuwa awamu inayofuata ni
ujenzi wa miundombinu ya kusambazia maji katika maeneo mbalimbali.
‘’Katika
awamu ya kwanza tumefanikiwa sana kuwekeza katika miundombinu mikubwa ya maji
hasa kutoa maji kwenye vyanzo vya maji ikiwemo chanzo cha maji cha Ruvu Chini
na Ruvu juu na mradi wa kuyatoa maji kutoka ziwa Victoria, sasa tunakwenda
awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya kusambazia maji hayo’ Amebainisha
Mhandisi Lwenge.
Ameongeza
kuwa awamu hiyo ya pili pia itahusisha uondoaji wa miundombinu chakavu katika
maeneo mbalimbali ambayo imekua ikisababisha upotevu wa maji kwa asilimia 47
pamoja na kuimarisha mifumo hiyo ili kutimiza lengo la Serikali la kufikia asilimia
95 ya kuwaunganishia maji wananchi
ifikapo mwaka 2020.
Akifafanua
kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji maeneo yanayozunguka ziwa Victoria amesema
kuwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 mradi wa maji katika vijiji 100 vilivyo
pembezoni mwa bomba kuu la maji linalotoka ziwa Victoria hadi Kahama na
Shinyanga itatekelezwa ili kuwawezesha wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo
kupata huduma ya maji safi.
Amesema
mradi wa kuvipatia maji vijiji hivyo utakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma
ya maji kwenye vijiji 40 vilivyotambulika katika Halmashauri za Misungwi,
Kwimba, Shinyanga na Msalala, Nansio, Geita na Buselesele pamoja na uboreshaji wa miundombinu
ya maji katika jiji la Arusha na mkoa wa Morogoro, Rukwa na Sumbawanga chini ya
ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ufaransa.
Aidha,
kuhusu kilimo cha Umwagiliaji Mhe. Lwenge amesema kuwa Serikali imeanzisha Tume
ya Umwagiliaji itakayokuwa na jukumu la kujenga mifumo na miundombinu ya maji
pamoja na kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalam kwa wananchi katika maeneo ya
kilimo.
Ameeleza
kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 ,Serikali imetenga kiasi cha shilingi
Bilioni 39 ili kuiwezesha sekta hiyo
kufanya vizuri na kuwaondoa wakulima kwenye kilimo kinachotegemea mvua pekee
kwa kuwa na kilimo endelevu cha umwagiliaji na kutoa wito kwa wananchi kuanza
kuvuna maji ya mvua katika maeneo yao.
Kuhusu ujenzi wa mfumo wa kusafisha maji taka katika jiji la Dar es
salaam amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itatekeleza mradi huo
kwa kuweka mfumo mpya wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa katika
jiji la Dar es salaam ili kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi
Amesema mradi huo utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji taka kwenye maeneo ya katikati ya jiji, ujenzi wa miundombinu mipya ya kupitishia maji hayo katika maeneo ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
"Serikali tumeanza kutekeleza mpango wa kupanua mfumo wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa na watumiaji maji , usanifu wa awali wa miradi mipya ya majitaka umekamilika,kazi inayoendelea ni usanifu wa kina ili kuweza kupata vitabu vya zabuni na michoro itakayotumika kumpata mkandarasi wa ujenzi" Amesisitiza Mhandisi Lwenge.
Amesema kuwa kupitia mpango huo bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika na badala yake maji hayo yatapelekwa katika mtambo mpya wa kisasa wa kusafisha majitaka ambapo maji hayo ambayo yatakua yamesafishwa yatauzwa na kutumiwa katika shughuli mbalimbali za upozaji wa mitambo na umwagiliaji.