WAFANYABIASHARA WA VIUMBE PORI HAI WAOMBA HURUMA YA RAIS MAGUFULI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Ally Daud-MAELEZO
WAFANYABIASHARA wa viumbe pori hai wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kufungulia biashara ya viumbe hao kutokana na kusitishwa Machi mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii Jumanne Magembe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Viumbe pori hai Bw. Salim Mussa amesema kuwa wanamuomba Mh. Rais Magufuli aingilie kati swala hilo na kupata ufumbuzi wa kudumu wa kuendelea na biashara hiyo ya viumbe kwa maendeleo yao na uchumi wa taifa.
“Tunakuomba Mh. Rais Magufuli uingilie kati swala hili na kutupatia ufumbuzi wa kudumu ili kuendlea na biashara ya viumbe pori hai bila ya usumbufu wa mara kwa mara kwani biashara hii ipo kwa mujibu wa sheria , taratibu na kanuni za nchi” alisema Bw. Salim.
Aidha Bw. Salim amesema kuwa maamuzi hayo yanaweza kusababisha hasara kubwa kwa jumuiya ya wafanyabiashara wa viumbe hivyo na uchumi wa nchi kwa ujumla kwani  muongozo haujatolewa tangu kusitishwa kwa biashara hiyo mwezi machi mwaka huu.
Kwa upande wake Msemaji wa wafanyabiashara wa viumbe pori hai Bw. Enock Balilemwa amesema kuwa kusitishwa kwa biashara hiyo imepunguza kiwango cha ajira kwa kiasi cha watanzania milioni moja ambao asilimia 95 wanaishi vijijini.
“kusitishwa kwa biashara hii ya viumbe pori hai imefanya watanzania takribani milioni moja hasa wakazi wa vijini asilimia 95 kukosa ajira jambo ambalo linapelekea wananchi hao kukosa uwezo wa kujikimu kwa maisha ya kila siku” alisema Bw. Balilemwa.
Biashara hiyo ya viumbe pori hai inayojumuisha Vyura, wadudu, ndege,mijusi na tumbili, zoo na mashamba ya wanyapori ilianza kabla ya uhuru sambamba na leseni zingine za uwindaji wa kitalii ambayo mpaka sasa inatambulika kwa sheria namba 5 ya mwaka 2009.

Serikali kukipandisha kituo cha afya cha Laela kuwa hospitali ya Wilaya

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukarabati kituo cha afya cha Laela kilichopo mkoani Rukwa ili kikidhi vigezo vya kuwa Hospitali ya Wilaya ikiwa ni moja ya jitihada za kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya zilipo.

Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Suleimani Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kwela Mhe. Ignas Malocha aliyehitaji kujua ni lini kituo hicho cha afya kitapewa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya.

Mhe. Jafo amesema kuwa ni uamuzi wa muda mrefu wa Serikali kuiweka Hospitali hiyo kuwa ya Wilaya na ndiyo sababu ya kufanya jitihada za kukiongezea uwezo kituo hicho kwa kujenga wodi nyingi pamoja na kutoa kibali cha kuajiri watumishi wapya kwani kwa sasa kituo hicho kina upungufu wa watumishi .

Amefafanua kuwa hadi sasa kuna baadhi ya majengo ambayo tayari yameshakamilika ambayo ni jengo la upasuaji wa dharura, wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji pamoja na wodi ya mama wajawazito.

“Kwa sasa kituo cha afya cha Laela hakina miundombinu inayokidhi sifa za kuwa Hospitali ya Wilaya ila kutokana na kupanuka kwa Mji huo na kuongezeka kwa watu wanaohitaji huduma katika kituo hicho tumeamua kukiboresha ili kifikie hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya”, amesema Jafo.

Ameongeza kuwa kwa sasa huduma za rufaa kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika kituo hicho zinatolewa kupitia magari ya kawaida ya Halmashauri kutokana na ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa lakini Wizara ina matarajio ya kutenga fedha ya kununulia gari hilo katika Bajeti ya mwaka 2017/2018.

Aidha, Mhe. Jafo amethibitisha kuwa kituo hicho kimetengewa jumla ya shilingi 9,358,100 katika Bajeti ya fedha ya mwaka huu ambayo itagharamia kununua dawa na vifaa tiba vitakavyorahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi wa eneo hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea kuipitia mikataba ya makampuni binafsi ili kuangalia namna ya kushirikiana nao katika kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba katika Hospitali na vituo vya afya nchini.


 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa