KAMPUNI YA TANWAT YATOZWA FAINI YA MILIONI HAMSINI KWA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Na Lulu Mussa
Njombe

Wadau wa Mazingira wametakiwa kufuata Sera, Kanuni na Tararibu katika kuendesha shughuli zao.  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba ameyasema hayo leo Mkoani Njombe alipokuwa katika mwendelezo wa ziara ya kutembelea Mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kujionea hali ya mazingira na kutoa maelekezo stahiki.
Waziri Makamba ametoza faini Kampuni ya TANMAT kwa kuikuka Sheria ya Mazingira inayokataza upandaji wa miti ndani mita sitini kutoka katika chanzo cha maji. "Kampuni hii imevunja sheria hivyo hamna budi kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe mfano na kwa wengine" alisisitiza Waziri Makamba.
Kampuni hiyo imeagizwa kulipa faini hiyo ndani siku saba na endapo watakiuka hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Waziri Makamba pia ameiagiza Kampuni hiyo kuondoa miti hiyo ambayo si rafiki kwa mazingira mapema iwezekanavyo na kuagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwapa 'Restoration Order"  kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na upandaji wa miti Bw. Joseph Shirima amekiri kupokea barua zizoelekeza kusitisha uharibifu huo wa Mazingira katika chanzo cha Mto Mbukwa ambacho kinasambaza maji kwa wakazi wengi wa Wilaya ya Wanging'ombe.
Aidha, Waziri Makamba ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Njombe kupitia Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachi kuacha kulima bustani za mbogamboga pembezoni mwa mito.
Dkt. Nchimbi alimfahamisha kuwa kwa sasa kuna kikundi kijulikanacho kwa jina la "Jerusalemu" kinachotoa mafunzo kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira ambapo lengo ni kuanzisha vituo kama hivyo vya mafunzo kwa Halmashauri zote za Mkoa huo.
Waziri Makamba alitembelea na kuona "vinyungu" ambavyo awali vilikua vikilimwa kando ya mito na kwasasa vimehamishiwa majumbani, katika kuunga mkono jitihada hizo njema Waziri Makamba amechangia mifuko Hamsini ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa litakalotumika kutoa mafunzo zaidi ya kilimo.
Waziri Makamba Waziri Makamba anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya mazingira nchini, hii leo amewasili katika Mkoa wa Mbeya.

SHULE YA SEKONDARI YA MALANGALI YAPATA NEEMA KUTOKA KWA MALANGALI ALUMNI ASSOCIATION (MAAS)


Hawa ndio baadhi ya wanafunzi waliowahi kusoma katika shule ya sekondari ya Malangali wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya  kuwasili katika shule hiyo na kukaangalia mazingira ya shule hiyo na kutafuta njia za kutatua baadhi ya changamoto kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania
mkurugenzi wa kampuni ya Yono action mart Yono Kevela ambaye ni mlezi wa kundi la Malangali Alumni association (MAAS) akizungumza mbele ya wanafunzi wa shule ya sekondari Malangali na kuwaeleza jinsi gani shule hiyo ilivyowapa mafanikio hadi sasa walipofikia.



 na fredy mgunda,Iringa

Wanafunzi waliowahi kusoma shule ya sekondari ya Malangali iliyopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamewataka vingozi,wafanyabiashara,wakulima na wajasiliamali mbalimbali walinufaika na elimu kutoka shule ya malangali kurudisha fadhila katika shule hiyo.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa kampuni ya Yono action mart Yono Kevela ambaye ni mlezi wa kundi la Malangali Alumni association (MAAS) alisema kuwa maendeleo aliyoyapata sasa ni kutoka na shule ya mangali hivyo ameamua kurudi na kuisadia shule hiyo. 

“Wafanyakazi na viongozi mblimbali tunatakiwa kuboresha mazingira na miundombinu ya shule tulizosoma ili kuendeleza na kukuza elimu ya hapa nchini tanzania.” Alisema Kevela

Kevela amesema kuwa shule nyingi walizosoma viongozi,wafanyabiasha na wajasiliamali mbalimbli zinahitajika kukarabatiwa hivyo amewataka wadau wote kuzikumbuka shule walizosoma.

Naye Padre wa kanisa la kikatoriki mkoani mbeya Telesipholi Tweve aliwakata wanafunzi mbalimbali waliosoma katika shule kongwe kurudisha upendo katika shule hizo kwa kuwa ndio chanzo cha mafanikio yao ya leo.

“Leo nimerudi katika shule hii ya malangali kuja kusaidia kutatua changamoto ambazo zipo katika shule hii ukizingatia kuwa shule hii inauchakavu wa majengo na miundombinu hivyo sisi kama MAAS tumeanza kwa kukarabati ukumbi ambao utakuwa na faida kwao kwa kutumia kwenye sherehe na kukodishwa pia”.alisema Tweve

Kwa upande wake mwenyekiti wa Malangali Alumni association (MAAS) Paul Mng’ong’o alisema kuwa wameanza kuisaidia shule ya Malangali muda mrefu kwa kuwa tayari wameshakarabati ukumbi wa shule,wamewanunulia tv na king’amuzi kwa ajili ya habari na wanaendelea kutatua matatizo ya shule hiyo.

“Hebu angalia sisi tuliosoma hapa tumepata mafanikio lakini shule yetu bado ipo pale pale na inazidi kuchakaa hivyo inatulazimu kuchangishana ili kurudisha fadhila kwa kuwa wengi wetu tumepata mafanikio makubwa kutoka shule hii,tunaviongozi wengi,matajili wengi ,wakulima wakubwa sana hapa nchini wote wamesoma katika shule hii”.Alisema Mng’ong’o

Lakini pia Mng’ong’o alisema kuwa lengo la kundi la Malangali Alumni Association kuunganisha wanafunzi wote waliowahi kusoma shule ya secondary ya Malangali na kuweza kupeana malengo na kusaidiana pale wanapokwama kimalengo.

Shule ya Malangali ni kati ya shule kongwe ambazo viongozi mbalimbali katika serikali,taasisiza Umma na sekta walijengewa msingi wa kwanza wa maisha.

kaika mwaka wa bajeti huu serikali imetenga bajeti ya kukarabati shule kongwe zipatazo thelethini na saba (37) jambo ambalo wananfunzi hao wameomba serikali kuharakisha utekelezaji wake.  
K

Sera ya Ajira kupitiwa upya



SERIKALI inapitia upya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili kuangalia changamoto zilizomo. Mapitio hayo yatakamilika kabla ya Desemba, mwaka huu, lengo likiwa kutoa fursa kwa wadau kushirikiana na serikali katika suala zima la ajira nchini.
Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Ally Msaki alisema hayo jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kuongeza kuwa hatua ya kuipitia sera hiyo, inatokana na kuwapo kwa mabadiliko mbalimbali.
Alisema, serikali itafanya kila linalowezekana, kuhakikisha kunakuwepo sera, sheria pamoja na kanuni rafiki, kwa maendeleo ya programu zinazokuza ujuzi na ajira kwa vijana.
“Sera hiyo imekuwa ikipitiwa na Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini (Repoa) na tayari ripoti inayoelezea hali halisi, imeshajadiliwa na wadau na sasa hivi wanaandika sera yenyewe,” alisema Msaki.
Alisema wadau, wameshiriki katika kuipitia sera hiyo, kazi kubwa imefanyika na imeangalia changamoto na matatizo mbalimbali yanayoikabili sera hiyo ili itakapokamilika itatoa mwanga wa wadau wengine kushirikiana na serikali katika suala la ajira.
Msaki alisema serikali itaendelea kusimamia sera hiyo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi, kwa lengo la kuweka msisitizo katika kuandaa mazingira na kutoa elimu ya ufundi stadi katika ngazi mbalimbali kuendana na mahitaji ya soko la ajira na hatimaye kuongeza ajira nchini.
Kuhusu mipango ya serikali katika juhudi za kukuza ajira, ni pamoja na kuimarisha utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya vijana ambao unalenga kuwasaidia vijana kujiajiri na kuwapa mikopo ya masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali.
Alisema serikali itajikita katika kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvukazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020, kulingana na mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia 2016/17 hadi 2020/21.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa