SERIKALI YAWAOMBA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO VITA DHIDI YA WAHUJUMU MIUNDOMBINU YA MAJI, YAAHIDI KUONGEZA HUDUMA YA UPATIKANAJI WA MAJI MIJINI NA VIJIJINI.



Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson LwengeAkizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa na Televisheni ya Taifa (TBC)

Na. Aron Msigwa -Dar es salaam.
 
Serikali imesema kuwa itaendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watendaji wa sekta ya maji watakabainika kujihusisha na vitendo vinavyohujumu miundombinu ya maji kutokana na maslahi binafsi na kusababisha wananchi kukosa huduma maji katika maeneo mbalimbali nchini. 

Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema baadhi ya watumishi wasio waaminifu wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu na miradi mipya ya maji inayoanzishwa na Serikali ili waweze kunufaika na biashara ya kuuza maji. 

Amesema Wizara yake imekwisha kuwasimamisha kazi Mameneja 9 waliokuwa wakihushishwa na wizi wa kimtandao wa maji katika maeneo mbalimbali hususani katika jiji la Dar es salaam.

‘’ Nimewasimamisha Mameneja karibu 9 waliokuwa wakihusika na wizi wa kimtandao wa maji na kuwafanya wananchi wakose huduma hii kwa muda mrefu, ninaomba wananchi watoe ushirikiano ili tuwakomeshe wahujumu hawa, tunahitaji kuondoa hali hii kwa kuwa maji ni uhai wa Taifa’’ Amesisitiza 

Amewaomba wananchi waendelee kutoa taarifa  kwa mamlaka zinazohusika pale watakapobaini vitendo vinavyoihujumu sekta hiyo ili ili hatua stahiki kwa wahusika zichukuliwe ikiwemo kuwafikisha mahakamani wale wote wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa maji na kuwafanya wananchi wawe na malalamiko ya kukosa maji.

Akizungumza kuhusu vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya maji nchini amesema kuwa kiasi cha shilingi Trilioni moja kimetengwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini.

Amesema lengo la Sera ya Maji ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi ndani ya umbali wa mita 400 jambo ambalo linaendelea kutekelezwa na kuongeza kuwa tayari miradi ya maji 1200 kati ya 1800 mijini na vijini imekamilika na kuwezesha asilimia 72 ya wananchi vijijini kupata maji na asilimia 80 ya wananchi walio mijini kupata huduma hiyo.

Amesema Serikali imejitahidi kuwekeza kwenye miundombinu mikubwa ya maji katika maeneo ya mijini hasa katika mikoa yenye idadi kubwa ya watu ikiwemo jiji la Dar es salaam, Mbeya, Mwanza na miji mingine na kuongeza kuwa awamu inayofuata ni ujenzi wa miundombinu ya kusambazia maji katika maeneo mbalimbali.

‘’Katika awamu ya kwanza tumefanikiwa sana kuwekeza katika miundombinu mikubwa ya maji hasa kutoa maji kwenye vyanzo vya maji ikiwemo chanzo cha maji cha Ruvu Chini na Ruvu juu na mradi wa kuyatoa maji kutoka ziwa Victoria, sasa tunakwenda awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya kusambazia maji hayo’ Amebainisha Mhandisi Lwenge.

Ameongeza kuwa awamu hiyo ya pili pia itahusisha uondoaji wa miundombinu chakavu katika maeneo mbalimbali ambayo imekua ikisababisha upotevu wa maji kwa asilimia 47 pamoja na kuimarisha mifumo hiyo ili kutimiza lengo la Serikali la kufikia asilimia 95  ya kuwaunganishia maji wananchi ifikapo mwaka 2020.   

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji maeneo yanayozunguka ziwa Victoria amesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 mradi wa maji katika vijiji 100 vilivyo pembezoni mwa bomba kuu la maji linalotoka ziwa Victoria hadi Kahama na Shinyanga itatekelezwa ili kuwawezesha wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo kupata huduma ya maji safi.

Amesema mradi wa kuvipatia maji vijiji hivyo utakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma ya maji kwenye vijiji 40 vilivyotambulika katika Halmashauri za Misungwi, Kwimba, Shinyanga na Msalala, Nansio, Geita na  Buselesele pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya maji katika jiji la Arusha na mkoa wa Morogoro, Rukwa na Sumbawanga chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ufaransa.

Aidha, kuhusu kilimo cha Umwagiliaji Mhe. Lwenge amesema kuwa Serikali imeanzisha Tume ya Umwagiliaji itakayokuwa na jukumu la kujenga mifumo na miundombinu ya maji pamoja na kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalam kwa wananchi katika maeneo ya kilimo.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 ,Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 39 ili kuiwezesha sekta  hiyo kufanya vizuri na kuwaondoa wakulima kwenye kilimo kinachotegemea mvua pekee kwa kuwa na kilimo endelevu cha umwagiliaji na kutoa wito kwa wananchi kuanza kuvuna maji ya mvua katika maeneo yao.

Kuhusu ujenzi wa mfumo wa kusafisha maji taka katika jiji la Dar es salaam amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itatekeleza mradi huo kwa kuweka mfumo mpya wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa katika jiji la Dar es salaam ili kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi

Amesema mradi huo utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji taka kwenye maeneo ya katikati ya jiji, ujenzi wa miundombinu mipya ya kupitishia maji hayo katika maeneo ya Ilala, Kinondoni na Temeke.

"Serikali tumeanza kutekeleza mpango wa kupanua mfumo wa uondoaji na usafishaji wa majitaka yanayozalishwa na watumiaji maji , usanifu wa awali wa miradi mipya ya majitaka umekamilika,kazi inayoendelea ni usanifu wa kina ili kuweza kupata vitabu vya zabuni na michoro itakayotumika kumpata mkandarasi wa ujenzi" Amesisitiza Mhandisi Lwenge.

Amesema kuwa kupitia mpango huo bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika na badala yake maji hayo yatapelekwa katika mtambo mpya wa kisasa wa kusafisha majitaka ambapo maji hayo ambayo yatakua yamesafishwa yatauzwa na kutumiwa katika shughuli mbalimbali za upozaji wa mitambo na umwagiliaji.

HAPA NA PALE MKOANI NJOMBE

Picha kwa hisani ya Mitandao mbalimbali
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa