NANI NI NANI URAIS: MCHUNGAJI CHRISTOPHER MTIKILA: MWENYEKITI DP

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mchungaji Christopher Mtikila akichangia hoja wakati wa Bunge Maalumu la Katiba
Historia yake
Mchungaji Christopher Mtikila ni Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP) ambacho kina usajili wa kudumu hapa Tanzania. Alizaliwa mwaka 1950 (ana umri wa miaka 65) mkoani Njombe, Kusini mwa nchi yetu.
Kwa bahati mbaya, hadi nachapisha uchambuzi huu sikupata taarifa za elimu ya Mtikila kwani hakuwa mwepesi kutoa ushirikiano mwezi mmoja uliopita na baadaye alisafiri kwenda  nje ya nchi na kurejea wakati nikiwa katika hatua za mwisho za uhariri.
Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa Kanisa la Kipentekoste la Full Salvation. Lakini pia kwa muda mkubwa wa maisha yake amekuwa anajihusisha na harakati za haki za binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo kiitwacho “Liberty Desk”. Kanisa lake ni moja ya makanisa machache hapa Tanzania yenye vitengo vya namna hiyo.
Umaarufu wa Mtikila ulikua sana mwanzoni mwa miaka ya 1990 kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu kile anachokiita “uhujumu wa uchumi unaofanywa na watu ambao anawaita magabacholi” na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika Mahakama za Tanzania, ni kati ya mambo machache yaliyomfanya asikike kila kona ya nchi.
Kwa muda mrefu, chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar. Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na siyo Tanzania. Hata hivyo, ilimpasa abadili msimamo wake katika miaka ya hivi karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama kutoka Zanzibar (kama sheria ya uchaguzi inavyotaka) ndipo kikapata usajili wa kudumu.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba. Mwaka 2004 pia alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala. Kwa ujumla maisha yake yamekuwa ni ya harakati muda wote, akipambana awezavyo, akisimama kidete inavyowekana na akijikuta matatani kila uchwao.
Mchungaji Mtikila amemuoa Georgia na wana watoto.
Mbio za ubunge
Mwaka 1997, Mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM wakati huo, Horace Kolimba aliitwa na Kamati Kuu ya chama chake mjini Dodoma kwenda kujibu mashtaka ya ndani ya chama juu ya kauli ambazo alikuwa akizitoa kwamba “CCM imepoteza mwelekeo”, baadhi ya viongozi wa chama chake walimchukulia kama msaliti na wengine wakimuona kama mtu aliyethubutu kusema ukweli bila kumhofia Nyerere. Hata hivyo, Kolimba alifariki hukohuko Dodoma katika siku ambazo alikuwa akihojiwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipotangaza uchaguzi mdogo, ndipo Mtikila alikihama chama chake cha DP akajiunga na Chadema na kuomba ridhaa ya kugombea. Mtikila ni mzaliwa wa Ludewa na alifanya hivyo kwa sababu chama chake cha DP kilikuwa kimenyimwa usajili.
Uchaguzi ulifanyika Mei 25, 1997 na kumpa ushindi mgombea wa CCM Profesa Chrispin Haule Che Mponda ambaye alipata kura 20,111 dhidi ya 8,386 za Mtikila. Mgombea wa NCCR ambayo haikuwa imejijenga vilivyo Ludewa, Barnabas Kidulile, alipata kura 1,271.
Baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mtikila alisikika akihitilafiana na Chadema hadharani huku akitoa shutuma nzitonzito, akafukuzwa kwenye chama hicho na ndipo akaendelea kuwekeza nguvu kwenye mipango ya kukamilisha usajili wa chama chake.
Mbio za urais
Mtikila alianza harakati za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya DP. Alikuwa kati ya wagombea 10 katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 0.27 ya kura zote, akiwa nyuma ya Jakaya Kikwete wa CCM (asilimia 80.28), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (asilimia 11.68), Freeman Mbowe wa Chadema (asilimia 5.88), Augustine Mrema wa TLP (asilimia 0.75) na Dk Sengondo Mvungi wa NCCR (asilimia 0.49).
Hakugombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010 na chama chake hakikuweka mgombea. Hata mwaka huu, hajaweka msimamo wake wazi japokuwa taarifa za ndani ya chama hicho zinaonyesha kuwa kinaweza kusimamisha mgombea na huenda mtu huyo akawa Mtikila.
Nimemuweka katika orodha hii kwa sababu tayari anatajwa kuwa na sifa, vigezo na hata historia ya mapambano inayompa nafasi ya kuweza kusimama mbele ya Watanzania kuomba uongozi wa juu.
Nguvu yake
Jambo la kwanza ambalo bila shaka linampa nguvu ikiwa ataingia kwenye kinyang’anyiro cha urais ni umaarufu wake. Mtikila ni maarufu, si kwa watu wenye umri wa zamani tu, lakini pia hata kwa vijana wadogo wa sasa. Ni vigumu ikiwa Mtanzania yeyote anayefuatilia masuala ya siasa katika nchi au habari mara kwa mara na asimjue. Ni kiongozi anayejishughulisha na mambo mengi mno na harakati zilizopitiliza na kwa mwanasiasa anayetaka nafasi ya juu, umaarufu unaweza kuwa karata muhimu, la msingi tu umaarufu huo vichwani mwa watu uwe na maana ya kumuona kama “mtu muhimu” katika hatua zake.
Lakini jambo la pili linalompa nguvu na sifa zaidi, ni kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya mara kwa mara, ya kufungua kesi za masuala ambayo Serikali inakuwa imewanyima raia kwa muda mrefu. Mara nyingi katika siasa za Afrika, kesi za kuishtaki Serikali kwa masuala ambayo yanaonekana kuwa makubwa huwa linaonekana kama jambo hatari hata kwa usalama wa mhusika.
Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya na polisi na nyinginezo. Hebu tujiulize, ni vyama vingapi vya siasa vimewahi kuwa na “uthubutu” huo?
Mtikila alishinda kesi ya mgombea binafsi na aliiweka Serikali kwenye njia panda kwa asilimia 100. Katika suala hili yeye ni mtu wa kujivunia na kama upiganaji wa kiwango hiki peke yake ndiyo ungekuwa tiketi ya urais, basi tayari angestahili tuzo hiyo bila mjadala.
Hakuna mwanasiasa mwingine yeyote hapa Tanzania aliyewahi kupambana na Serikali mahakamani kila kukicha kama Mtikila, hayupo!
Lakini jambo la tatu linalompa nguvu na sifa ni misimamo ya kipekee. Mtikila hajali anapokuwa ana ajenda zake na misimamo yake na mara nyingi misimamo hiyo huwa ni ya kipekee hata kama ni mibaya kiasi gani, yeye huisimamia na kubakia nayo hata kama wenzake wote watamkimbia. Nakumbuka tulipokuwa Bunge Maalumu la Katiba, alikuwa na ajenda ya kusimamisha Bunge lile lisifanye kazi kwa sababu limeanza kinyume cha sheria na halina hadhi ya kutunga katiba ya nchi. Pamoja na wanasheria wakongwe kuwa na mawazo tofauti naye, bado alishikilia msimamo wake na aliondoka kwenda Dar es Salaam kwa minajili ya kufungua kesi husika (sina taarifa jambo hili lilipoishia
Hata baadaye, vyama vinavyounda Ukawa vilipoamua kutoka bungeni, Mtikila aliunga mkono uamuzi huo na alisisitiza kuwa yeye anafanya kazi na umoja huo kwa suala la katiba, sijapata taarifa za hatima yake katika kuendelea kuwa ndani ya Ukawa, lakini ninachojua ni kwamba misimamo hii ya Mtikila kuna wakati imekuwa na tija kubwa, si kwake tu, bali kwa Taifa zima.
Udhaifu wake
Udhaifu wa kwanza wa Mtikila ni utoaji wa “kauli tata” ambazo kuna nyakati zinaudhi na kuamsha hasira ya upande uliotuhumiwa. Mtikila ana tabia ya kuzungumza mambo magumu na mkishindana anaweza akakudharau na hata kukupa jina baya ambalo hukuwahi kufikiri kuwa unaweza kuitwa au kupewa. Mara kadhaa amewahi kusikika akitoa shutuma kali kwa viongozi wa nchi na hata vyama vya upinzani. Sifa hii si nzuri kwa mtu ambaye ana ndoto au anaotewa kushika uongozi wa juu wa nchi siku moja.
Lakini jambo la pili ambalo naliona ni udhaifu pia, hupenda kushughulikia mambo ya hatari peke yake na wakati mwingine bila kufanya kazi ya kutosha kuwaelimisha wananchi na vyombo vya habari na kutafuta hali ya kupewa uzito na mioyo ya wananchi na wadau. Tabia hii ya kuamka na ajenda nzito mkononi na kulazimisha ajenda anayotoa iungwe mkono ghafla bila kuwaandaa wananchi, siyo jambo zuri kisiasa.
Kuna masuala ya msingi anayapigania na yanapotoshwa na vyombo vya habari na wanasiasa wa vyama vingine kwa sababu tu hakufanya kazi ya siasa ya kuyatangaza, kuomba ushirikiano wa wenzake. Ili uwe kiongozi mzuri una wajibu wa kuwashirikisha watu waliokuzunguka ili uamuzi mkubwa unaotaka kufanya uungwe mkono. Kujifanyia peke yako kunakuwa hakuna tija kubwa kwa masilahi mapana ya wote.
Mwisho, Mtikila amekuwa akitoa kauli zinazodhaniwa kuwa ni za kibaguzi na hili haliko “uvunguni”, amefanya hivyo mara nyingi mno katika mikutano yake na hata mbele ya vyombo vya habari. Kuna wakati amekuwa akisikika hadharani akiwatuhumu Wahindi kwa lugha za kibaguzi, anawaita “magabacholi”, lakini pia kuna wakati amewahi kulalamikiwa hata na nchi jirani ya Rwanda kwa namna alivyowahi kuyashutumu makabila makubwa ya nchi hiyo kwa kauli za kibaguzi.
Kiongozi mmoja wa juu wa Serikali nimewahi kumsikia akisema kuwa alipokutana na kiongozi mmoja wa juu wa Rwanda, baada ya salamu akamuuliza kiongozi huyo “who is Reverend Mtikila”? (Mchungaji Mtikila ni nani?). Mtikila siyo tu kuwa anaipa chemsha bongo Serikali nchini, hata huko nje wanaumiza vichwa juu yake na hili siyo suala la kujivunia kama kweli nchi inatafuta viongozi watakaoimarisha uhusiano na nchi za jirani.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo mawili yanaweza kukifanya chama cha DP kimpitishe:
Jambo la kwanza ni ikiwa hakina mtu mwenye sifa za kumfikia. Jambo hili lina uwezekano mkubwa wa kutokea kwa sababu ndani ya DP, mwanasiasa pekee maarufu na anayefahamika ni Mtikila. Kuna wanasiasa wengine kadhaa vijana lakini hawajafanikiwa kufahamika na kwa sababu mgombea urais huuzwa kwa wananchi, kumuuza mtu mgeni katika siasa za ushindani ni vigumu, ndiyo maana anaweza kupitishwa yeye mwenyewe ili kukiweka chama chake kwenye nafasi ya kipekee.
Lakini jambo la pili linaloweza kumvusha ni kwa sababu tayari ana uzoefu na kuihitaji nafasi hii mwaka 2005. Hili liko wazi, kwamba DP inajua umuhimu wake kama Mtanzania aliyewahi kuzunguka huku na kule na akapigiwa zaidi ya kura 30,000. Kwa mtu asiyejua siasa anaweza kuzidharau kura hizo lakini wanaojua mambo ya siasa wanafahamu ilivyo kazi kubwa hata kupata kura chache tu kwenye kinyang’anyiro hicho. DP inaweza kumpitisha ili akaongeze wigo wa kura nyingine zaidi.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo la kwanza linaloweza kumwangusha ni ikiwa chama chake kitamtazama kama mtu mwenye misimamo mikali na anayeweza kukikosesha chama hicho nafasi katika uchaguzi wa kisasa ambao unahitaji zaidi kuzungumzia “masuala” na siyo watu au shutuma. Kama nilivyoeleza, kwa kiasi kikubwa majukwaa ya Mtikila hutumika kushutumu watu, Serikali na vitu kama hivyo. Ni mara chache mesikika akihutubia kuhusu ajenda za kuzisimamia kwa mapana. DP inaweza kuhitaji kuondokana na staili hizo na ikatafuta mwanzo mpya kwa kumweka mtu mwingine.
Lakini pili, matokeo ya mwaka 2005 ambayo yanaweza kutafsiriwa kama hayakuwa mazuri, yanaweza kuchukuliwa kama sababu ya kutompa nafasi, ili apatikane mwanachama mwingine ambaye ataweza kukipa zaidi nafasi chama hicho.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Asipochaguliwa atakuwa na masuala kama matatu:
Kwanza ni kuendelea na uchungaji katika kanisa lake ambalo linaendelea kukua na hivyo linahitaji usimamizi. Nadhani kazi hii ya uchungaji ni moja ya mambo muhimu kwake na ameshaizoea vilivyo huku akichanganya na kudai haki za wananchi. Nauona uchungaji kama karata muhimu pia ya kuendeleza karama yake ya siasa na nina hakika ataendelea na kazi hii.
Lakini mpango wa pili nadhani ni kuendelea kuongoza DP. Hadi sasa sijamsikia akitamka kuwa atastaafu muda mfupi ujao, nadhani bado atakuwamo katika chama alichokiasisi na kwa sababu siasa za Kiafrika ziko namna hii kwa kiasi kikubwa, naona ataendelea kugombea na kuwa mwenyekiti kama jukumu jingine.
Mpango wa tatu utaendelea kuwa harakati za ufunguzi wa kesi za kutetea wananchi na masuala makubwa ambayo yanakiuka kikatiba. Kazi hii imo moyoni na kwenye damu yake na nina hakika kwamba ataifanya kufa au kupona, hii ndiyo imejenga sifa yake na lazima atakwenda nayo mbele zaidi kama moja ya mipango yake.
Hitimisho
Mtikila, ni mwanasiasa mtata, anayethubutu, mwenye misimamo. Si rahisi kumfafanua hivihivi. Maisha yake ni harakati tokea asubuhi hadi jioni, ukipishana naye anavyopenda kupanda bajaji au pikipiki akiwahi mahakamani (siyo wakili) na ukimuona anavyosimamia masuala makubwa katika nchi, huwezi kuamini kuwa mtu wa aina yake ndiye hasa mwenye uwezo huo.
Kuongoza kanisa (uchungaji), kuongoza chama cha siasa na kushinda mahakamani kupambana na Serikali kwenye kesi kubwa kabisa ni mambo mchanganyiko mno na yanathibitisha kuwa mwanasiasa huyu angepata chama chenye mtandao mkubwa katika nchi na akatumia uwezo wake vizuri kwa masilahi mapana ya Taifa, angekuwa na mchango mkubwa kwa jamii kuliko ilivyo sasa. Namtakia kila la heri kwenye safari yake ambayo naamini ina maana kubwa na walau ina mchango wa kipekee katika mapambano ya kidemokrasia hapa Tanzania.
Chanzo:Mwananchi

150 KORTINI KWA KUJIANDIKISHA MARA MBILI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGAKURA KWA MFUMO MPYA BVR‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema watu 152 watafikishwa mahakamani mkoani Njombe kutokana na kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration Kit’ (BVR).
Aidha, imeeleza kuwa kata 130 zimeongezeka kutokana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kufanya mabadiliko ya kiutawala katika kata, vijiji,vitongoji na Mitaa hivyo kulazimu NEC kuhairisha kwa wiki moja uandikishaji wa daftari uliokuwa ukianza jana kwa baadhi ya mikoa.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk Sisti Cariah alisema hayo jana wakati akielezea kuahirishwa kwa wiki moja uandikishaji hadi Juni 16 mwaka huu kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara.
Akizungumzia suala la watu kujiandikisha mara mbili, alisema katika mkoa wa Njombe ambao Daftari hilo liko tayari na wiki ijayo litawekwa wazi kwa siku tano na kisha kufanyiwa marekebisho kwa siku moja na wamebaini watu 152 waliojiandikisha mara mbili.
Alisema watu hao wametenda kosa la jinai na watashtakiwa, huku akitoa onyo kwa watu kuacha kufanya hivyo kwani mashine za BVR zinagundua wanaojiandikisha zaidi ya mara moja.
Alisema wataweka wazi baadhi ya watu waliojiandikisha mara mbili kwenye mikoa yote, ambayo iko tayari.
Alisema mpaka sasa tayari wamepokea madaftari yaliyokamilika ya uandikishaji kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma huku uandikishaji huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 50 na wanatarajia kukamilisha uandikishaji mwezi Julai.
Akizungumzia suala la mipaka ya kiutawala, yaliyofanywa na Tamisemi, Cariah alisema ilifanyika wiki mbili zilizopita katika mikoa mbalimbali, jambo lililosababisha kusitisha uandikishaji katika mikoa hiyo huku mikoa ambayo tayari uandikishaji umefanyika watarekebisha wakati wa kuweka wazi daftari.
“Katika kupiga kura lazima kitambulisho kioneshe kata anayokaa mtu kwa mabadiliko haya yamefanya kata kubadilika na kuongezeka 130 hivyo kufanya madiwani watakaopigiwa kura kuongezeka hivyo kata kuendana na kitambulisho,” alisema.
Alisisitiza kuwa kutokana na changamoto hiyo mikoa hiyo mitano, itaanza uandikishaji pamoja na mikoa ya Tanga na Morogoro Juni 16 mwaka huu na baadaye Juni 25,mwaka huu wataanza uandikishaji katika mkoa wa Pwani.
Alisema sasa wanatumia Mashine za BVR 8,000 walizokuwa wanahitaji pamoja na vipuri vyake vyote ziliwasili yangu mwezi uliopita.
Alisema katika mkoa wa Dar es Salaam uandikishaji utaanza Julai2 mwaka huu kwa kutumia BVR zaidi ya 3,000, ambazo kila moja ina uwezo wa kuandikisha watu 120 na hiyo itatokana na kuwa mikoa nane, uandikishaji utakuwa umemalizika na zote kutumika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
“Jijini Dar es Salaam sehemu zenye watu wengi kutakuwa na mashine hizo nyingi huku vituo vyote, vikifunguliwa kwa mara moja ikifuatiwa na Zanzibar, ambapo wataandikisha waliokosa sifa za kuandikishwa katika Daftari la ukaazi kwa ajili ya kupiga kura ya kumchagua Rais wa Muungano”alisema.
Akizungumzia changamoto ya watu kusubiri kwa muda mrefu katika vituo vya kujiandikisha, alisema hiyo inatokana na kuwa Printa za kusafisha picha zinatakiwa kubadilishwa kila baada ya wapigakura 400 kutokana na vumbi na muda huo wtau uona kama mashine zimeharibika lakini ni utaratibu wa kawaida.
Cariah alisema uandikishaji umekamilika kw amikoa mitano ya Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa na imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wanaendelea katika mikoa 12 sasa ambayo ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Dodoma, Singida, Kigoma, Kagera, Simiyu, Mwanza, Geita na Shinyanga.
Akizungumzia mafanikio ya mikoa hiyo kuwa takwimu ilikuwa kuandikisha wapigakura 518,230 na waliandikisha watu 529,224, Mtwara walitakiwa 732,465 waliandikisha 727,565, Ruvuma wapigakura 783,296 waliandikishwa 826,779 na Iringa wapigakura 524,390 waliandikishwa 526,006.

WANANJOMBE NA IRINGA WAJITOKEZA KWA WINGI KUMDHAMINI WAZIRI MEMBE ILI AGOMBEE URAIS WA TANZANIA‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Bernard Membe (kulia) akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Njombe, waliofika kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Njombe Jana, kwa ajili ya kutia saini fomu za kumdhamini ili ateuliwe kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya chama hicho, ambapo aliweza kupata wadhamini zaidi ya 360.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Bernard Membe akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Iringa, waliofurika kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Iringa mjini Jana, kwa ajili ya kutia saini fomu za kumdhamini ili ateuliwe kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya chama hicho, ambapo aliweza kupata wadhamini 317.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa