Home » » TUSHIRIKIANE KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI - NAGU

TUSHIRIKIANE KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI - NAGU

 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu.
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, amesema kazi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi si ya serikali pekee hivyo wadau malimbali na taasisi za fedha zinapaswa kutumia sehemu ya faida yake kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
 
Aliyasema hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha kazi baina yake na Wajumbe wa Baraza la Uwezeshaji la Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), akiwamo Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i  Issa na Mwenyekiti wa Bodi, Omari Issa.
 
Baadhi ya ajenda kwenye kikao hicho ilikuwa ni kupata na kujadili taarifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi Tanzania, fedha za mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira na uzinduzi wa mkakati wa sekta mbalimbali wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.
 
Dk. Nagu alitoa wito kwa NEEC kukutana na Chama cha Wenye Benki nchini na kuwashawishi waone umuhimu wa kutumia sehemu ya faida yao katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kwenye miradi ya biashara.
 
“Tangu mfuko wa uwekezaji uanzishwe, haukui na sababu ni kwamba unategemea chanzo kimoja tu serikali, sasa lazima tuondokane na mawazo ya kuitegemea serikali tu tuwe na vyanzo vingine vya mapato na tukikutana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, naamini watakuwa tayari kuchangia jitihada hizi za serikali,” alisema.
 
Aidha, alisema vikundi vya kuweka na kukopa maarufu kama vicoba, vikisimamiwa na kuendeshwa  vizuri, vitakuwa mkombozi mkubwa wa uchumi wa Tanzania na kuwakwamua wananchi wengi kuondokana na tatizo la umaskini kwa kuanzisha miradi.
 
Waziri Nagu alisema kuna ushahidi wa baadhi ya wananchi walioanzisha na kusimamia vizuri vicoba na hivi sasa wana mitaji mikubwa inayowawezesha kufanya biashara kubwa na kuongeza mitaji.
 
“Kuna mfano dhahiri wa kikundi cha watu 30 ambao wamefanikiwa kukusanya Sh. milioni 300 ndani ya muda mfupi, sasa kama watu 30 tu wanaweza kukusanya kiasi hicho cha fedha, si jambo la kubeza, inaonyesha kwamba tukivisimamia vizuri vitawakomboa wananchi wengi kiuchumi,” alisema.
 
Alisema iwapo wananchi watajiunga na vicoba na kuwekeza kwenye miradi inayowapa faida ni dhahiri wananchi wengi watakata tamaa ya kujiunga na vikundi hivyo lakini kama vitakuwa vikijiendesha kwa hasara hakuna atakayejiunga.
 
"Kwa bahati nzuri vicoba ni watu wanaofahamiana na wanaoaminiana na wakipata mwongozo mzuri naamini kabisa watafika mbali zaidi, ndiyo sababu nimeona umuhimu wa kumjumuisha Mwenyekiti wao Taifa, Devotha Likokola, kwenye baraza hili, kwa sababu naamini kabisa kupitia Vicoba tunaweza kufika mbali zaidi kiuchumi,” alisem Dk. Nagu.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa