Home » » ‘WANAUME MNAOPIGWA NA WAKE ZENU JITOKEZENI’

‘WANAUME MNAOPIGWA NA WAKE ZENU JITOKEZENI’

 
 Ni nadra kusikia mwanamume akilalamika kuwa amepigwa na mke au mwenza wake. Suala hilo ni adimu zaidi katika nchi za Afrika hasa zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zimefunikwa na blanketi la mfumo dume.
Kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni woga, aibu na kasumba ya mfumo dume, wanaume wanaonyanyaswa wamekuwa wakificha aibu hiyo na kuendelea kubaki katika unyanyasaji huo.
Kutokana na ongezeko la matukio ya wanaume kunyanyaswa na wake au wenza, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania, (Tawla) kimetoa wito kwa wanaume kujitokeza ili kupata msaada wa kisheria pindi wanaponyanyaswa.
Mwenyekiti wa asasi zisizo za kiserikali za katiba na jinsia, (Zec) zinazoratibiwa na Tawla, Victoria Mandari anasema matukio hayo ni mengi lakini wanaume wamekuwa wakiyafanya kuwa siri pengine kwa kuona aibu.
“Wanaume watafute chama kitakachowasaidia kutetea haki zao na kutengeneza hata sheria ambazo zitawasaidia kupata haki zao,” anasema. Anasema sheria zinasema kuwa asiwepo mwanandoa anayemnyanyasa mwenzake kijinsia, hivyo basi hata wanaume nao hawatakiwi kunyanyaswa.
“Tatizo ni kuwa wanaume hawajitokezi wanaponyanyaswa, waseme ili wasaidiwe,” anasema.
Matukio ya wanaume kunyanyaswa na wake zao yameendelea kutokea huku wanaume wakidai kuwa unyanyasaji huo unachochewa na wingi wa vyama, asasi, na mashirika yanayotetea haki za wanawake pekee.
Mwaka jana, Naibu Kamishna wa Polisi, Adolphina Chialo alisema wanaume wengi sasa wanakwenda kushtaki katika madawati ya kijinsia ya polisi pale wanaponyanyaswa.
Inaelezwa kuwa hata wanawake wanaowanyima unyumba waume zao bila sababu maalumu nao wanafanya unyanyasaji wa kijinsia.
Kamishna Chialo anasema wapo wanaume wanaofika vituo vya polisi wakiwa na majeraha baada ya kupigwa na wake zao.
Katiba Inayopendekezwa
Pamoja na unyanyasaji kwa wanaume, wanasheria hao walizungumzia Katiba Inayopendekezwa na kusema kuwa licha ya kupingwa na taasisi nyingi za kijinsia na kisheria nchini, kwa upande wao imezingatia masuala ya jinsia ambayo awali, hayakutambuliwa katika Katiba ya sasa.
Mandari anasema maoni yaliyotolewa na chama hicho katika Katiba Mpya yalifanyiwa kazi.
“Tumeona mambo mengi ambayo tuliyasema wakati wa kukusanya maoni kwa mfano, Katiba Inayopendekezwa sasa inatambua kabisa masuala ya ndoa, umri sahihi wa ndoa na umiliki wa mali,” anasema.
Anasema Katiba ya mwaka 1977 iliruhusu ndoa kwa msichana wa miaka 14 suala analosema liliwanyima mabinti haki ya kusoma na kuchochea unyanyasaji wa kijinsia.
“Ile sheria haikuwa nzuri kabisa, hebu fikiria mtoto mdogo anaingia katika ndoa wakati hata maumbile yake bado ni madogo, hata kura hawezi kupiga lakini anakuwa mke wa mtu,” anasema
Anasema zaidi jinsi Katiba Inayopendekezwa ilivyoyafanyia kazi maoni yao yaliyohusu haki za wanawake na kusema kwa sasa kuna marekebisho ya sheria ya kimila ambayo katiba ya zamani haikumtambua mtoto wa kike kama mrithi wa mali isiyohamishika jambo ambalo kwa sasa halipo.
Aidha, anasema sheria nyingi zilizokuwapo katika katiba ya zamani zilionekana kukinzana. Kwa mfano, sheria hizo hazikufafanua mtoto ni nani na ana haki gani na kwa upande mwingine zikiruhusu mtoto kufunga ndoa.
“Tulitumia fursa hii vyema kwa sababu tulijua kabisa katiba ni moyo na ikitengenezwa basi kuibadili huwa ni kazi vigumu lakini tunashukuru maoni yetu yalifanyiwa kazi,” anasema
Katika kuhakikisha wanatoa maoni bora ya katiba, Tawla walitembelea nchi za Afrika Mashariki ili kujifunza jinsi ambavyo nchi hizo ziliunda katiba yenye manufaa hasa kwa upande wa haki za kijinsia.
“Tulijifunza kwa kina kabla ya kutoa maoni yetu, hatukutembea Afrika Mashariki tu, bali tulifika hata Afrika Kusini nia ilikuwa ni kuhakikisha mwanamke anatambulika na anakuwa na fursa katika katiba hii,” anasema.
Mwanasheria, Cecilia Assey anawaasa wanawake kuacha woga pindi wanapokumbana na unyanyasaji kutoka kwa waume, wenza au wanajamii kwani sheria zipo.
“Hapa tunapata elimu kuhusu katiba na masuala ya jinsia lakini baada ya mafunzo haya tutaendelea na kazi ya kuwasaidia wanawake wanaokumbana na changamoto katika jamii,” anasema.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa