Home » » BRN IMEWAJALI WANAFUNZI, SI WALIMU- CWT NJOMBE

BRN IMEWAJALI WANAFUNZI, SI WALIMU- CWT NJOMBE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani Njombe mkoani Njombe kimeitaka serikali kufanya tafiti za kutosha katika miradi yake ukiwemo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), wakidai unawazidishia mzigo wa kuwajibika bila kuongezwa ujira.

Pia chama hicho kimeitaka Serikali kusitisha biashara huria ya vitabu vya kiada kutokana na kukinzana kwa baadhi ya vipengele hivyo; kusababisha ugumu katika ufundishaji.

Katibu wa CWT wilayani humo, Bi. Salama Lupenza, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika risala yake aliyoisoma Siku ya Walimu Duniani iliyofanyika mjini Makambako.

Alisema kama Serikali itashindwa kudhibiti hali hiyo iwe inahariri vitabu hivyo na kuvigonga mihuri ili kuwahakikishia walimu.

Aliongeza kuwa, yapo mafanikio katika BRN, lakini wanasikitishwa na mradi huo kutowaangalia walimu badala yake wamewaongezea majukumu bila kuongeza ujira jambo linaloweza kuhatarisha maendeleo ya elimu kwa wanafunzi nchini.

"Waandaaji BRN hawakufanya utafiti wa kutosha kwa sababu kama unashindwa kumwezesha mwezeshaji wa mradi, usitegemee majibu mazuri...mradi huu umewaangalia zaidi wanafunzi si mwalimu ambaye bado ana vilio vingi kama mshahara mdogo, pesa za likizo; hivyo Serikali iwe inatushirikisha katika mipango yake," alisema.

Kwa upande wake, mgeni rasmi mkuu wa wilaya hiyo, Bi. Sara Dumba, aliwataka walimu waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu yakiwemo mavazi.

Aliwataka waache tabia ya kukopa katika taasisi za fedha ambazo zimekuwa haziweki wazi masharti yao wakati Serikali ikiendelea kutatua kero zao.

"Elimu ni msingi bora wa maisha, mwalimu ni kioo cha jamii na Serikali kwa upande wake, itaendelea kutatua kero zenu pamoja na kuboresha mazingira mazuri ya kazi.

"Naamini siku moja kelele zote zitaisha kutokana na mipango jinsi ilivyo, miradi ya BRN imewekwa kwa ajili ya jamii iweze kupunguza matatizo mbalimbali," alisema Bi. Dumba.

Sikujua Joel ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, alisema ili kila mtoto aweze kupata elimu bora, ipo haja ya Serikali kutochanganya siasa na elimu hasa kwenye vitabu vya ufundishia, kuuchunguza upya mradi huo na kuufanyia marekebisho

Chanzo;Majira

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa