Home » » WANAUME WATAHIRIWA KUEPUKA UKIMWI

WANAUME WATAHIRIWA KUEPUKA UKIMWI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SERIKALI wilayani hapa inaendelea kuwafanyia tohara wanaume wasiotahiriwa ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kuzuia kuongezeka kwa maambukizi mapya ya Ukimwi kwa wakazi wake.
Hatua hiyo imetokana na wataalamu kubaini kuwa, kuna uhusiano mkubwa kwa wanaume wasiotahiriwa na ongezeko la maambukizi mapya ya Ukimwi.
Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa wilaya hiyo ina asilimia 6.1 ya maambukizi na Mkoa wa Njombe ndiyo unaoongoza kitaifa kwa kuwa na wastani wa asilimia 7.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Madaha, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusu mkakati wa kupambana na maambukizi mapya ya ugonjwa huo ambapo kwa sasa umepata mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa Madaha, Wilaya ya Ludewa ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa kwa Ukimwi na kunatakiwa juhudi kubwa na za makusudi kupunguza tatizo hilo ikiwamo kuongeza elimu ya uelewa wa athari kwa wananchi.
Alieleza kuwa, hapo mwanzo mapambano dhidi ya Ukimwi yalikuwa magumu na tatizo kubwa lilionekana kuwepo kwa idadi kubwa ya wanaume wasiotahiriwa hivyo kwa namna moja na nyingine kuchangia kuongezeka kwa tatizo.
Madaha alisema, pamoja na hatari ya kupata Ukimwi kwa urahisi, lakini pia kutofanyiwa tohara kwa wanaume kunasababisha maambukizi ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake jambo ambalo ni hatari kwa afya na kusababisha vifo.
Aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuwa waangalifu na nyendo zao na kujiepusha na tabia inayoweza kuwasababishia kupata maambukizi mapya kwa kuepuka kufanya ngono zembe.
Chanzo;Habari Leo 

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa