Home » » TANZANIA INAVYOSHINDWA KATIKA KISWAHILI KIMATAIFA

TANZANIA INAVYOSHINDWA KATIKA KISWAHILI KIMATAIFA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
 
Wako waandishi na watafiti ambao ni wageni na hupenda zaidi kujifunza Kiswahili. Ukiwauliza kwa nini wanapenda Kiswahili, wanajibu kuwa ni lugha ya pekee isiyobanwa na dhana za kikabila na kieneo, inavuka mipaka ya nchi na kuwa ni ya kimataifa.
Mgeni mmojawapo ni Pete Muhunzi (jina la kupanga) ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika. Ni Profesa mstaafu wa historia na anafanya utafiti wa masuala ya lugha katika jamii na hasa Kiswahili.
Alifafanua kuwa sababu ya kutambuliwa kwa Kiswahili kuwa ni lugha ya kazi katika vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika (AU) ni hatua muhimu katika historia ya lugha hiyo. Uamuzi uliotolewa wa kukifanya Kiswahili kuwa ni lugha ya kazi, uliotokana na kukosekana kwa lugha nyingine za Kiafrika zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa mfano, lugha kama Kiigbo, Kiyoruba na Kihausa zote zikiwa ni za Afrika Magharibi na zinavuka mipaka ya nchi. Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) uliamua kuteua moja ya lugha za Kiafrika na kupendelea kukiteua Kiswahili.
Hatua ya kukiteua Kiswahili ilitokana na uamuzi uliofanyika katika kikao cha Mawaziri wa Utamaduni wa Umoja wa Nchi Huru za Afrka nchini Mauritius mwaka 1988. Mawaziri wa Utamaduni waliibua wazo la kupata lugha moja ya Kiafrika itakayotumika pamoja na lugha za kazi, ambazo ni za kikoloni yaani Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Pendekezo la mawaziri wa utamaduni la kutumia Kiswahili kuwa ni lugha ya Kiafrika na ya tano katika vikao vya OAU ni uamuzi wa kipekee.
Pendekezo hilo liliwasilishwa katika kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika huko Addis Ababa na lilikubaliwa.
Kwa kuwa Tanzania ni kitovu cha lugha ya Kiswahili na kina vyombo kadhaa vya kukikuza na kukiendeleza katika ngazi mbalimbali za jamii ikiwamo katika shughuli za Serikali, shuleni na vyuoni, iliteuliwa kusimamia na kutekeleza suala hili.
Hatua ya kwanza ni kuwatambua wafanyakazi waliohitimu chuo kikuu wenye digrii ya kwanza na waliosomea lugha ya Kifaransa.
Kwa maana hiyo, waliochaguliwa walikuwa wakifahamu Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili, lugha zilizokuwa zikitumika katika vikao vya OAU. Ilibidi kuwaandaa wataalamu katika fani za wakalimali na wafasiri ili waende kupata taaluma ya juu ya ukalimani na tafsri, ili watakaporejea kutoka masomoni wapelekwe Addis Ababa kutekeleza majukumu yao kwenye shughuli za kazi.
Je, hali ilikuwaje baadaye. Hapo awali ilibidi waandaliwe vijana waliosomea lugha katika ngazi ya shahada ya kwanza ili kupelekwa kujiendeleza katika taaluma hizi. Serikali ya Ufaransa ilikubali kugharimia mafunzo ya vijana hawa kwa safari na mafunzo. Kwa bahati nzuri waliteuliwa vijana wanne kwenda kusoma Ufaransa kwa mwaka mmoja. Baada ya kurejea nchini waliripoti Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Jambo la kushangaza ni kuwa wizara husika haikuwajali, hivyo wakaanza kujitafutia kazi wao wenyewe katika nchi za nje. Mmoja alikwenda Burundi katika Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu, mwingine alikwenda Ivory Coast katika Shirika la Uchumi la ECOWAS, Afrika Magharibi.
Tanzania imekosa nafasi ya kuwapatia vijana wake ajira ya uhakika. Hivi sasa huduma za ukalimani na tafsiri zinafanyika kwa mtindo wa kazi za muda (part time), badala ya kuwapo kwa wafanyakazi wa kudumu
Sasa, ipo haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Wizara ya Utamaduni, Vijana na Michezo kuwa na makubaliano ya kulikabili suala hili kwa pamoja na kurejesha nchi katika hadhi iliyopewa huko awali.
Kutokana na Tanzania kushindwa kutekeleza mapendekezo ya OAU, tutajilaumu wenyewe. Hii siyo mara ya kwanza kwa Tanzania kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa kuhusu lugha ya Kiswahili. Soma makala yajayo..
 Chanzo:Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa