Home » » RC AHIMIZA UWEKEZAJI CHUMBA CHA MAITI

RC AHIMIZA UWEKEZAJI CHUMBA CHA MAITI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MKUU wa Mkoa (RC) wa Njombe, Kapteni Mstaafu, Assery Msangi, amekaribisha watu binafsi, mashirika na taasisi yoyote kujitokeza kusaidia ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Kibena kutokana na kilichopo kuwa katika hali mbaya hivi sasa.
Kapteni Msangi, aliyasema hayo wakati akikabidhiwa msaada wa taa maalumu mbili za kufanyia upasuaji kwenye chumba cha upasuaji cha hospitali hiyo iliyopo mjini hapa, uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), wenye thamani sh milioni 9.
Msangi, alitoa rai kwa yeyote ambaye atakuwa tayari kufanya kazi ya kuwekeza kwenye chumba cha maiti, hatakuwa na kipangamizi.
Aliipongeza NSSF kwa msaada huo, lakini akatoa rai kwa shirika hilo, taasisi na watu binafsi, kufikiria namna ya kuweza kusaidia kujenga chumba cha maiti kwenye hospitali hiyo ya Kibena.
“Kwa niaba ya wananchi wangu na viongozi wa Mkoa wa Njombe, napenda kuwashukuru NSSF kwa msaada huo, lakini tunalo tatizo kubwa hivi sasa la mochwari, na mochwari hivi sasa hazijengwi na serikali, bali zinajengwa na mtu binafsi, taasisi na shirika lolote,” alisema Msangi.
Alisema endapo watajitokeza kuwekeza kwa kujenga chumba cha kuhifadhia maiti, kutasaidia kupata faida ya haraka na yenye manufaa.
“Mochwari na mila zetu ni mahali nyeti sana, lakini nataka niseme kwamba hili Katibu Tawala mliangalie, kwani zinajengwa na watu binafsi au taasisi, kwa sababu ukiweka maiti nane au kumi, maana yake utakuwa unamdai maiti hela kwa kila siku, ni biashara nzuri tu,” alisema Msangi.
Alitoa mfano kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Makamba, aliporuhusu biashara ya majeneza wengi waliona kama ni biashara ya ajabu, lakini hivi sasa imekuwa ni muhimu na isiyokuwa na shaka kwa jamii.
“Wapo walimfuata Makamba na kumwambia sasa mkuu hii si balaa, majeneza yanauzwa barabarani kama mashati, akawaambia muda wake ukifika mtaona umuhimu wake, ukienda hospitali ya KCMC pale, ile wamejenga wenyewe, lakini ile wameibinafsisha, kuna mtu anafanya shughuli pale, ukilaza maiti unalipia sh 5,000 au 10,000 kwa ‘night’, hivyo nataka nitoe wito kwa mashirika na watu binafsi wajitokeze kujenga.
“Ni biashara ambayo haina ubishi wala mapatano, kwa kawaida mfiwa hana mapatano au nipunguzie, huwa hamna mapatano ya kupunguziana bei, ni eneo ambalo ni zuri la biashara, hivyo watu wajitokeze kujenga, Watanzania wenye moyo na kuguswa na tatizo hili, wajitokeze kujenga hospitali yetu.”
Meneja wa NSSF Mkoa wa Njombe, Godwin Mwakalukwa, alisema shirika lao limetoa msaada huo, baada ya kuguswa na tatizo la ukosefu wa taa maalumu ya kufanyia upasuaji kwenye chumba hicho
 Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa