Home » » WARSHA YA UBORESHAJI WA KILIMO CHA APPLES MAKETE KWA MAAFISA KILIMO YAFUNGULIWA

WARSHA YA UBORESHAJI WA KILIMO CHA APPLES MAKETE KWA MAAFISA KILIMO YAFUNGULIWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba+255765056399.
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akizungumza wakati akifungua warsha kwa wataalamu wa kilimo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Makete hii leo. 
Mwezeshaji kutoka shirika ka TAHA Bw. Isaac Ndamanhyilu akizungumza kwenye warsha hiyo. 
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akizungumza na wataalamu wa kilimo wa kata na vijiji vya wilaya ya Makete. 
Wataalamu wakifuatilia mafunzo hayo. 
 Mwezeshaji Manfred Bitala akiwawezesha washiriki wa warsha hiyo.
Na Edwin Moshi
Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe imedhamiria kuinua kilimo cha matofaa maarufu kama apples, ili kiweze kuinua uchumi wa wakulima pamoja na wilaya kwa ujumla

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili kwa mabwana na mabibi shamba wa kata na vijiji, Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro amesema wilaya imeanza kutekeleza agizo la rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara wilayani hapo kuwa ni lazima kilimo cha apple kiwe cha biashara wilayani Makete

Mh. Matiro amesema mafunzo watakayopatiwa maafisa hao wa kilimo, wanatakiwa kuyafuata na kwenda kuyatekeleza kwa vitendo katika kata na vijiji vyao ili mabadiliko yaanze kuonekana na ndiyo maana halmashauri imeshirikiana na shirika la TAHA kuwapatia mafunzo ya namna ya kuboresha kilimo hicho katika maeneo wanayotoka

Amesema kwa kuwa jambo hili halihitaji masihara anatarajia kuona mabadiliko mara moja pindi mafunzo hayo yatakapo malizika kwa kwenda kuwaelekeza wakulima kitu cha kufanya ili apples zizalishwe kwa wingi na kwa ubora unaohitajika kwani hilo linawezekana kwa mujibu wa utafiti ambao umefanyika wilayani hapo

Mh. Matiro amesisitiza pia badala ya wananchi kupanda miti mingi ya mbao kwa sasa wanatakiwa wabadilike na wapande miti ya matunda hasa apples kwa kufuata elimu ya wataalamu hao wa kilimo ambayo wamepatiwa katika mafunzo hayo 

Kwa upande wake Bw. Isaac Ndamanhyilu kutoka shirika la Tanzania Hoticultural Association maarufu kama TAHA ambao ni watoaji wa mafunzo hayo, amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuongeza uzalishaji wa apples pamoja na uuzaji wa matunda hayo

Amesema kwa wilaya ya Makete imekuwa ikizalisha matunda hayo kwa wingi lakini hakuna kumbukumbu zinazoonesha kama uzalishaji huo upo Makete, na pia hakuna taarifa zinazoonesha kama wilaya hii ni miongoni mwa maeneo ndani ya Tanzania yanayozalisha apples

Bw. Ndamanhyilu amesema kufuatia kukosekana kwa kumbukumbu hizo, ndiyo maana wameamua kushirikiana na halmashauri kuhakikisha elimu inatolewa kwa mabwana shamba na mabibi shamba na wao wawaongoze wakulima kulima kilimo cha kisasa ili matunda hayo yazalishwe kwa wingi na yenye ubora unaotakiwa tofauti na ilivyo sasa

"Kulikuwa kuna maonesho fulani jijini Arusha, na mgeni rasmi alikuwa Rais Kikwete na alibahatika kuona apples pale, na alipoambiwa kuwa zinazalishwa Makete kwa kweli alishangaa, na ndiyo maana alisema atafika Makete kujionea, na kweli alifika na amesisitiza kilimo hiki kiwe cha biashara na ndio maana tunatoa hii elimu kwenu" alisema

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Manfred Bitala amewaasa mabwana na mabibi shamba hao kubadilika kwani wapo baadhi ya wataalamu hao wamekuwa wakihubiri elimu bila kufanya kwa vitendo jambo linalowakatisha tamaa wakulima

"Yaani wakati mwingine ukiliangalia shamba la mabwana na mabibi shamba nia aibu, yaani unakuta shamba la mkulima linaubora kuliko la ninyi wataalam, sasa hii inakatisha tamaa, lazima ninyi muwe mfano wa kuigwa" alisema Bitala

Amesema wao wananafasi kubwa ya kuibadilisha hii nchi kutoka hapa ilipo na kuonekana mabadiliko makubwa na yenye tija katika sekta ya kilimo kama kila mmoja ataamua kufanya kazi yake ipasavyo

Katika mafunzo hayo wamefundishwa mambo mengi ikiwemo dalili na aina za magonjwa yanayoshambulia matunda, na namna ya kulima na kupata mazao mazuri zaidi ya ilivyo sasa

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa