SAKATA LA KUHAMISHWA MTENDAJI IGWACHANYA, WANANCHI WAMTAKA MTENDAJI WAO

*RC amtetea DC kuhamia Mdandu
Na Waandishi wetu
Wananchi wa Kata ya Igwachanya wanamlilia aliyekuwa Mtendaji wa Kata yao kwa maelezo kuwa alikuwa mchapakazi.
Taarifa ambazo Kwanza Jamii-Njombe imezipata zinasema Job Fute amehamishwa kutoka katika kata hiyo kimyakimya baada ya kulitaarifu gazeti hili juu ya tetesi zilizopo katika kata hiyo juu ya uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe kutokubali nyumba ya mbunge na kuamua kuanzia shughuli zake kata ya Mdandu.
Imefahamika baada ya Fute kuondolewa katika wadhifa wake kama mtendaji wa Kata ya Igwachanya, hivi sasa yupo mapokezi katika idara ya utumishi katika ofisi za Halmashauri kama adhabu.
Hata hivyo, katika mkutano na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kepteni (Mstaafu), Assery Msangi aliwaeleza wananchi wa Igwachanya kuwa, kitendo cha kuamua kutumia ofisi za Mdandu ni kuepuka matumizi mabaya ya fedha kwani ingeigharibu wilaya hiyo ya Wanging’ombe kiasi kisichopungua sh. 90 milioni kuikarabati shule waliyokuwa wamepewa na kanisa huko Igwachanya.
Msangi aliyetumia muda mwingi kuelezea kwa nini ofisi ya DC alisema “Maneno yamekuwa mengi, sasa ni wakati wa kufanya kazi…tumeshatengewa sh.2.5 bilioni kwa ajili ya kujenga ofisi.”
Hata hivyo aliwataka wakazi hao kukubali madhara yanayotokana na eneo lao kuwa makao makuu kama kubomolewa nyumba kutokana na upanuzi wa barabara na pamoja kuanza kulipia huduma kama maji.
Akizungumzia uhamisho wa ghafla wa mtendaji wa kata ya Igwachanya kwa kueleza ‘ukweli’, Shukuru Martin, mkazi wa eneo hilo amesema, muda mfupi wa Fute umekuwa na maendeleo ya haraka hasa uhamasishaji wa uchangiaji wa sekondari.
Alikwenda mbele na kuongeza, wakazi wa eneo hilo hawaoni jambo baya aliloeleza kwenye gazeti na kuongeza; “tunashangaa serikali ilivyokuja juu na kumwamisha kiongozi wetu tena bila hata kutuambia lolote. Sasa tutaona itakavyokuwa sababu hatutamkubali mtendaji yoyote atakayeletwa kwenye kata hii.”
Naye Athuman Kilamlya, mkazi wa Igwachanya amesema, uamuzi huo unaonesha pasipo shaka kwamba, serikali haiwapendi viongozi wanaopenda kusema kama taarifa za Fute alizotoa kupitia Kwanza Jamii-Njombe.
Hildegat Mwanyika alilaumu kitendo cha mkurugenzi kumhamisha ghafla mtendaji huyo bila kuangalia upande wa pili ambao ni wa wananchi kwani wanamjua utendaji wake na kumwondoa ni sawa na kuwarudisha wananchi nyuma kimaendeleo.
“Mkuu wa wilaya alibisha hodi hapa na tulimpokea kwa moyo mmoja sasa kwanini aondoke tena bila taarifa yoyote? Mtendaji aliongea kwa niaba yetu sasa kwanini mkurugenzi amwamishe bila hata kusikia lolote kutoka kwetu, kwa maana hiyo mkurugenzi pia hana nia njema na sisi na anakubaliana na yale ambayo yataendelea kuturudisha nyuma,” alisisitiza.
Igwachanya ni eneo lililopo Wanging’ombe na Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuwa litakuwa makao makuu ya wilaya. Kutokana na maandalizi duni ya kulifanya eneo hilo kuwa makao makuu, Mkuu wa wilaya hiyo, Esterina Kilasi aliamua kuweka ofisi eneo ya Mdandu kwa muda, jambo lililowatisha wakazi wa Igwachanya kuwa huenda alitaka kuhamia huko moja kwa moja.
Chanzo: Jamii Kwanza Njombe

MUONEKANO WA GAZETI LA 'KWANZA JAMII NJOMBE' TOLEO LA SEPTEMBA 3-19,2012

WAWILI MBARONI KWA KUKATAA KUHESABIWA MAKAMBAKO

Festus Pangani, Njombe Yetu
Jeshi la Polisi Mkoani Njombe linawashikilia watu wawili Athuman Saidi Kivanga Mkazi wa Mtaa wa Kawawa Mji wa  Makambako na Yasini Shaibu wa Kijiji cha Kipagamo Kwa Tuhuma za Kukataa Kuhesabiwa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani  Njombe ACP Fulgency  Ngonyani Amesema Watu Hao Wamekatwa Agosti 27 Mwaka Huu Majira ya Saa Tano Asubuhi Ambapo Watuhumiwa Hao Walikataa Kuhesabiwa Kwa Madai Kuwa Imani Zao Haziruhusu Kufanya Hivyo.
Kamanda Ngonyani Amesema Kitendo cha Kukataa Kuhesabiwa ni Kosa la Jinai na Kinyume cha Sheria na Kwamba Watuhumiwa Wamekamatwa Kwa Mahojiano Ikiwa ni Pamoja na Kuwaelimisha Juu ya Umuhimu wa Sensa na Endapo Watazidi Kukataa Watafikishwa Mahakamani.
Katika Tukio Jingine Kamanda Huyo Amesema Watu Wasiofahamika Wamevunja Nyumba ya Fredy Mtulua Mkazi wa Kijiji Cha Igagala Wilaya ya Wanging'ombe na Kuiba Pikipiki Moja Aina ya Skymark Yenye Namba za Usajili T 664 BNQ Yenye Thamani  Zaidi ya Shilingi Milioni Moja .
ACP Ngonyani Amesema Tukio Hili Limetokea Agosti 27 Mwaka Huu Majira ya Saa Nane Usiku na Hakuna Mtu Yoyote Aliyekamatwa Kuhusika na Tukio Hilo.
Hata Hivyo Jeshi La Polisi Mkoani Njombe Linaendelea na Upelelezi Juu ya Matukio Hayo Ambapo Amewataka Wananchi Kutoa Ushirikiano Kwa Kutoa Taarifa Kwenye Vyombo Vya Dola Ili Kuwabaini Watu Waliojihisisha na Vitendo Vya Uhalifu.
Blogzamikoa

ZOEZI LA SENSA LAINGIA DOSARI MATEMBWE, WALEVI, WAZURURAJI WAKAMATWA


Mwandishi wetu, Njombe Yetu
Zoezi la sensa ya watu na makazi mwaka 2012 linaloendelea nchi nzima limeingia dosari katika kijiji cha Matembwe kilichopo tarafa ya Lupembe Mkoani Njombe kutokana na baadhi ya wananchi kukimbia makazi yao.
Wananchi hao wamekimbia makazi yao kutokana na baadhi ya wanakijiji kukamatwa kwa kosa la uzururaji na kunywa pombe muda wa kazi jambo ambalo wanakijiji hao walilihusisha na zoezi la sensa.
“Kuna baadhi ya watu baada ya kuona makarani wa sensa hawafiki katika makazi yao kama walivyotarajia waliamua kutafuta sehemu ili kuwasubiri wawahesabu, wakaenda kukaa kilabuni na kuanza kunywa pombe, askari wa Lupembe wakawakamata” alisema mmoja wa wanakijiji wa Matembwe.
Kutokana na wananchi wengi kutouelewa vizuri utaratibu wa uendeshaji wa sensa ya mwaka huu, wengi wamejikuta wakiwa njiapanda na kushindwa kujua namna wanavyotakiwa kushiriki katika zoezi hilo, jambo lililochangia wengine kukaa vijiweni wakingoja makarani kuwahesabu hapo.
Baadhi ya watu waliokamatwa na askari kutokana na kukaa vijiweni na kunywa pombe muda wa kazi wameeleza kuwa waliambiwa walipe faini kati ya shilingi elfu ishirini na elfu hamsini. 
Hata hivyo wananchi hao walilalamika kuwa pesa hizo zinazodaiwa kuwa ni faini zililipwa katika ofisi bubu hivyo kudhani wamefanyiwa uhuni.
“Wananchi wengine wameamua kukimbia zoezi la sensa kwa kudhani mwenyekiti wa sensa wilaya ndiye aliagiza wenzao wakamatwe na kuhisi ni uonevu umefanyika kwani waliokamatwa walikuwa wanasubiri kuhesabiwa kama wengine” alisema mwanakijiji huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Zoezi la sensa linaloendelea nchini sasa hivi limekuwa linakumbwa na vikwazo kadhaa ikiwemo madai ya ukosefu wa vifaa kama vile madodoso na baadhi ya makarani kususia kazi yao kutokana na madai ya posho yao huku wengine wakigomea kwa sababu za shinikizo na itikadi za kidini na kisiasa
Blogzamikoa

CHADEMA- Yapata Pigo Makete





Jumla ya vijana 47 waliokuwa wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) katika kata ya Tandala wilayani Makete wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha mapinduzi (CCM) katika mkutano wa hadhara uliofanyika katani hapo




Mmoja wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Nahom Dovisiana Sanga amesema alijiunga na Chadema mwaka 2011 lakini ahadi alizoahidiwa ikiwa ni pamoja na kusaidiwa kiuchumi haijatekelezwa na ndio maana ameamua kutoka kwenye chama hicho




Naye Imani Nyamike ambaye ni mkazi wa kata hiyo naye amesema kwa upande wake amejiona kama amepotea kutokana na kukosa ushirikiano kwa viongozi wa chama hicho hivyo kujiona mpweke tangu alipojiunga na chama hicho




“Mimi napenda kuwaasa vijana wenzangu ambao mmmedanganyika na CHADEMA ndugu zangu huu ni muda wa kurudi CCM, bibi na babu yangu wapo CCM, baba na mama yangu wapo CCM na mimi nimerudi CCM na nitakufa ndani ya CCM” alisema Nyamike




Akizungumza mkutanoni hapo Katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu amesema chama chake kimefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na vijana hao ya kujiunga na CCM na kusema wao kama chama cha mapinduzi wako tayari kuwasaidia vijana hao na kuwataka kujiunga na kuwa kikundi kimoja ili waweze kupatiwa mikopo ya riba nafuu ili wakuze mitaji ya bishara zao




Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya vijana kujiunga na vyama vyenye sera za uongo pasipo kujua madhara yanayokuja kuwapata mbele na huku akisistiza wananchi waliofika kenye mkutano huo kubakia chama cha mapinduzi ambacho kimepewa dhamana na wananchi kutekeleza sera zake ndani ya wilaya hiyo




“Ndugu zangu naomba niseme CHADEMA hawana adabu, hivi hakuna ambayo jema lililofanywa na CCM hata mkapongeza? Ninyi kila siku ni matusi tu majukwaani, hata kitendo cha wao kuishi kwa uhuru hadi sasa ni jitihada za serikali ya CCM, bado nalo si jema kwenu?” alisema Mtaturu




Mtaturu alitoa bendera za CCM kwa vijana hao na kusema kuwa kwa kuwa tukio hilo la kuhamia CCM limetokea ghafla, atajipanga ndani ya chama chake kufanya sherehe ya kuwakabidhi rasmi kadi za CCM na kuongeza kuwa zoezi hilo litafanywa na uongozi wa mkoa ama taifa




Katika hatua nyingine Mtaturu aliwataka wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa wanaoendelea na zoezi la kuhesabu watu katani humo kwani zoezi hilo bado linaendelea kwa siku saba mfululizo pamoja na wananchi hao kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya pindi tume ya kukusanya maoni itakapofika katani hapo




Naye diwani wa kata ya Tandala Mh. Egnatio Mtawa amewashukuru wananchi wa kata yake kwa ushirikiano wanaompa pamoja na kumuomba katibu wa CCm kusaidia kushughulikia suala la umeme wa gridi ya taifa kufika katani Tandala




Amesema huo ni mpango wa siku nyingi wa serikali kuhakikisha umeme unawaka Tandala hivyo anaombwa kusaidia kuimkumbusha serikali ili mpango huo ukamilike mapema





ASKARI MBARONI KWA KUTOROKA LINDO NA KUSABABISHA WIZI NYUMBANI KWA RC


Mwandishi wetu, Njombe Yetu

Jeshi la polisi Mkoani Njombe linawashikilia askari wawili waliokuwa lindo nyumbani kwa mkuu wa mkoa baada ya kutokea wizi usiku wa kuamkia siku ya sensa ambapo watu wasiofahamika waliingia nyumbani hapo na kuiba kompyuta mpakato moja,simu 3 mbili zikiwa nia aina ya Nokia ambazo ni mali ya watoto wa mkuu huyo wa mkoa.

Kamanda wa polisi kamishna msaidizi wa polisi Bw.Fulgence Ngonyani amesema, tukio hilo lilitokea wakati nyumbani hapo wakiwepo walinzi ambao ni askari polisi na kwamba kutokana na tukio hilo askari aliowataja kuwa ni mwenye namba G15414 PC Ombeni na wengine ni mwenye namba G 5455 PC Mohamed wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo.

kutokana na tukio hilo mkuu wa mkoa alisema kumekuwepo uzembe kwa askari polis wanaokuwepo Lindoni hapo kwani mara nyingi wamekuwa wakiacha lindo na kwenda kusikojulikana na kurudi wakiwa wamelewa, na kwamba kuna wakati wamekuwa wakitumia uda mwingi kulala na kuacha lindo.

Akizungumzia suala hilo Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kapteni mstaafu Aseri Msangi ametoa duku duku lake ama kero kuhusu askari hao kwamba tabia ya askari hiyo, ameiona si mara moja huondoka na kuacha lindo.

Amesema kuwa kuna siku alimkuta askari akiwa amelala ndani ya moja ya magari kati ya yaliyopo nyumbani hapo na kumwamsha akiwa fofo.

Blogzamikoa

FILIKUNJOMBE AKATAZA WANANCHI KUUZA MAHINDI BEI ‘CHEE’ YA SH.350

Festus Pangani, Nombe Yetu
Mbunge wa jimbo la Ludewa mh Deo Haule Filikunjombe amewataka wananchi jimboni humo kutouza mahindi katika msimu huu wa kilimo kwa bei ya shilingi 350 kwa madai kuwa hiyo inawakandamiza na kuwanyonya wakulima.

Akizungumza kwa njia ya simu Filikunjombe amesema serikali imekuwa ikiwanyonya wananchi wilayani Ludewa kwa kununua mahindi yao kwa bei kandamizi wakati katika mikoa mingine mahindi hayo yamekuwa yakinunuliwa kwa bei ya shilingi 380.

Amehoji kuwa kama mbolea ya ruzuku inayotolewa kwa wakulima katika msimu wa kilimo haitofautiani nchini,ni kwa nini kwa jimbo la Ludewa pekee mahindi kutoka kwa wakulima yanunuliwe kwa bei ya shilingi 350 tofauti na mikoa mingine, na kuhoji kuwa shilingi 30 ambayo ni ongezeko kwa mikoa mingine inapelekwa wapi.

Amesema katika taarifa yake  wakala wa ununuzi mahindi katika ghala la chakula  lililoko katika mji wa Makambako mkoani Njombe imebainisha kuwa wamelazimika kununua mahindi kwa bei hiyo kutoka kwa wakulima wilaya ya ludewa kufuatia miundo mbinu ya barabara kuwa mbovu hali inayopelekea gharama kubwa katika suala la usafirishaji.
Blogzamikoa
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa