WANANCHI LUDENDE WALIA UKOSEFU WAHUDUMU WA AFYA.


Festus Pangani, Njombe Yetu Blog
Wananchi wa Kata ya Ludende wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe wameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushindwa kupeleka wahudumu wa afya katika Zahanati Ludende hali inayosababisha adha kubwa kwa wakazi wa kata hiyo.
Pamoja na Zahanati hiyo kufunguliwa wakati wa maadhimisho ya miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania mwaka jana lakini hakuna mfanyakazi hata mmoja na kwamba majengo ya zahanati hiyo ikiwa ni pamoja na nyumba ya mganga mkuu vimetelekezwa.
Akiongea kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wananchi hao alisema kuwa haoni sababu ya kuwa na majengo mazuri yaliyojengwa kwa kodi ya wananchi bila ya kuwepo wahudumu wa afya huku wananchi wakiendelea kuumia.
Mtendaji wa Kata ya Ludende, Lezile Luoga alikiri kutokuwepo kwa mfanyakazi yeyote katika Zahanati hiyo na mpaka sasa hakuna maelezo ya kina yanayohusu upatikanaji wa wafanyakazi katika Zahanati hiyo.
Luoga alisema wananchi wamekuwa wakijitolea kufanya maendeleo ya ujenzi wa Zahanati hiyo cha kushangaza wamekuwa wakipata huduma za matibabu katika Zahanati za vijiji vya mbali wakati dhahanati yao iko katika ubora unaokubalika.
“Tumewahamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa zahanati hii hadi imekamilika lakini cha kushangaza Serikali imeshindwa kuleta wafanyakazi, hii inakatisha tamaa na wananchi wanaweza wasijitolee kufanya kazi za kimaendeleo” alisema Luoga.
Naye Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Ikovo, Menrufu Mgaya alisema ukosefu wa huduma ya afya umeleta usumbufu kwa wanafunzi wa shule yake hasa pale yanapotokea magonjwa ya milipuko yanayowakumba wanafuzi kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.
Blogzamikoa

BARABARA YA NJOMBE-LUDEWA YATENGEWA FEDHA


Festus Pangani, Dodoma

Hatimaye Serikali imesikia kilio cha Mbunge wa Ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (CCM) cha kuitaka barabara ya Njombe, kupitia Ludewa hadi Manda ijengwe kwa kiwango cha lami.

Akijibu Swali namba 264 bungeni jana, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Gerson Lwenge, alisema kufuatia ombi la Filikunjombe, katika mwaka huu wa fedha wa 2012/2013, tayari Serikali imetenga shilingi 1,600 millioni kwaajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo kwaajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.

“Aidha, katika kuhakikisha barabara ya Ludewa inatengenezwa na kupitika kwa urahisi,” alisema jumla ya shilingi milioni 800 zingine zimetengwa katika bajeti hii ya 2012/2013 kwaajili ya matengenezo maalum ya barabara kuu kwa kiwango cha changarawe.

 “Lengo ni kuifanya barabara ya Njombe - Ludewa iweze kupitika katika majira yote ya mwaka,” alisema Waziri Lwenge aliyekuwa akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi - Mhe. John Pombe Magufuli.

 “Ujenzi wa barabara ya lami toka Njombe, kupitia Ludewa hadi Manda ni nuru mpya ya matumaini kwa wana Ludewa wote,” alisema Bwn. Filikunjombe akiongeza kuwa “barabara ya lami itachochea kasi kubwa ya Maendeleo katika wilaya ya Ludewa.”

Filikunjombe amemshukuru na kumpongeza Dr. Magufuli kwa kuwafanya wana Ludewa nao wanufaike na matunda ya miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu. “Kwa niaba ya wananchi wa Ludewa ninakushukuru sana mhe. Waziri kwa kuitazama Ludewa kwa jicho la pekee,” alisema Filikunjombe. 

Katika mwaka 2011/2012 Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara, ilianza kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 1.5 Ludewa Mjini na ujenzi bado unaendelea.

Barabara ya Njombe – Ludewa – Manda yenye urefu wa km 212 ni barabara kuu itakayohudumiwa na wakala wa barabara – TANROADS - mkoa wa Njombe.

Blogzamikoa

Karibu Mkoa Mpya wa Njombe



Mkoa mpya wa Njombe
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa mipya Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya na Iringa.
Mwaka 2002 katika eneo hilo kulikuwa na wakazi 654,929 [1] katika wilaya zifuatazo: Makete (wakazi 106,061), Njombe (wakazi 420,348), Ludewa (wakazi 128,520).
Kutokana na hadhi mpya, wilaya ya Njombe imegawanyika kati ya ile ya mjini na ile ya vijijini. Pia imeanzishwa wilaya ya Wanging'ombe.
Makao makuu yako Njombe mjini.
Wenyeji wa mkoa ni hasa kati ya makabila yafuatayo: Wabena, Wakinga, Wapangwa, Wawanji, Wakisi na Wamanda.



 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa