TAKUKURU NJOMBE YAMNG'ANG'ANIA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA LUDEWA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ludewa Mhe. Matei Kongo

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani Ludewa mkoani Njombe jana imempandisha mahakamani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Matei Kongo na kusomewa mashtaka upya ya kuomba na kupokea rushwa kiasi cha shilingi 100,000 kati ya shilingi 300,000 alizokuwa akiomba


Akisoma upya mashtaka mbele ya Hakimu mkazi Wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna mwendesha mashtaka wa TAKUKURU mkoa wa Njombe Malekano Richard aliiambia mahakama ya Hakimu mkazi Wilayani hapa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi
12 mwaka huu katika bar na Hotel ya Merland Ludewa mjini.


Katika kosa la kwanza Bwana Malekano alisema mshtakiwa huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Luilo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa aliomba
kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Samsoni Mwaipugile ili aweze kumpa
upendeleo katika zabuni mbalimbali ikiwemo kusambaza kompyuta na tenda
za ujenzi wa majengo.


Malekano aliiambia mahakama kuwa kosa la pili linaangukia katika
kifungu namba 15(1)(A) cha taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa,
na kwamba kwa nyakati tofauti kati ya disemba mwaka jana na machi
mwaka huu mshtakiwa Kongo aliomba rushwa ya shilingi milioni tatu
ambapo machi 12 mwaka huu alipokea kiasi cha shilingi laki moja
kupitia kwa wakala wake Aidani Luoga zilizotolewa na Samsoni
Mwaipugile mkazi wa Dar-es salaamu.


Hata hivyo mshtakiwa Mathei Kongo mbele ya mahakama alikana kuhusika
na makosa yote yanayomkabili.


Aidha mwendesha mashtaka Marekano Richard aliiambia mahakama kuwa
upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kuiomba
mahakama ipange tarehe ya kusikilizwa.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi mei 9 mwaka huu itakapokuja kusikilizwa na
dhamana ya mshtakiwa itaendelea.


Mshitakiwa huyo amesomewa upya shitaka hilo kutokana na awali kufikishwa kimakosa katika mahakamani ya Mwanzo na kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo imelazimika kusomwa upya katika mahakama hiyo ya hakim mkazi wa wilaya ya Ludewa .
Habari kwa Hisani ya Francis Godwin
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa